header

nmb

nmb

Thursday, January 26, 2012

SERIKALI YASISITIZA,MADAKTARI WALIO KWENYE MGOMO KUREJEA KATIKA VITUO VYAO VYA KAZI.




Na. Aron Msigwa –MAELEZO





Serikali imewataka madaktari wote nchini walio kwenye mgomo kurejea katika vituo vyao vya kazi na kufanya kazi za utabibu ili kuokoa maisha ya wagonjwa.





Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hadji Mponda amesema serikali inatambua mchango walio nao wataalam wa afya katika utoaji wa huduma za afya nchini na inaendelea kuboresha maslahi yao.




Amesema serikali kwa kutambua mchango huo imekuwa ikiboresha maslahi yao na kuongeza nafasi za ajira kila mwaka kwa wataalam wenye sifa kutoka nafasi 1,677 za mwaka 2005/2006 hadi kufikia 9,391 katika mwaka huu wa fedha 2011/2012.





“Serikali inatambua mchango wa watumishi wa kada za afya nchini na ndio maana nafasi za ajira zimekuwa zikiongezeka kila mwaka hasa katika mwaka huu wa fedha 2011/2012”





Amefafanu kuwa madaktari kupitia Chama chao (MAT) wamewasilisha madai mbalimbali serikalini yakiwemo nyongeza ya posho ya kuitwa kazini baada ya kazi na madaktari kupewa nyumba za kuishi karibu na hospitali amesema kuwa serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuboresha maslahi hayo ili kuwawezesha wataalam hao kutekeleza majukumu yao ikiwemo ujenzi wa nyumba 8 za madaktari kwa wilaya 18 pamoja na kufanya maboresho ya posho.





“Serikali imepata fedha kutoka Mfuko wa Dunia(Global Fund) kwa ajili ya kujenga nyumba za madaktari na kwa kuanzia wilaya 18 zilizo pembezoni zimechaguliwa kujengewa nyumba 8 kila wilaya kama hatua ya kuboresha upatikanaji wa nyumba”






Kuhusu malipo ya udhamini kwa madaktari wanaochukua mafunzo ya uzamili,Kuhamisha madaktari bingwa wenye mikataba ya Ajira na Hospitali ya Taifa Muhimbili, Posho ya mazingira hatarishi na ajira za madaktari amesema kuwa baada ya serikali kupandisha hadhi ya hospitali za mikoa kuwa hospitali za Rufaa za mikoa kumekuwa na umuhimu wa madaktari hao kwenda kufanya kazi katika hospitali hizo na kuongeza kuwa idadi ya udhamini wa madaktari katika mafunzo ya uzamili imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.





Aidha kuhusu madai ya kutaka nyongeza za mishahara ya shilingi milioni 3.5 kwa mwezi Dkt. Mponda ameeleza kuwa mishahara ya watumishi serikalini hufuata miundo ya utumishi (Scheme of Service)iliyopo huku akibainisha kuwa muundo wa malipo ya watumishi wa umma katika sekta ya afya umeboreshwa.





“Lazima tukubali kuwa baada ya kuboreshwa kwa miundo ya utumishi wa umma wafanyakazi wa sekta ya afya hivi sasa wanapata mishahara mikubwa kuliko watumishi wengine serikalini” amesisitiza.

No comments:

Post a Comment