header

nmb

nmb

Wednesday, January 11, 2012

DAWA YA KUFUKUZANA NI KUWA NA MGOMBEA BINAFSI-TENDWA


Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa (kulia), sasa ameanza kupigia kampeni haja ya kuwepo mgombea binafsi ili kukuza demokrasia nchini.

Pia, Tendwa amesema kuwepo mgombea binafsi itakuwa moja ya njia ya kudhibiti ‘fukuza fukuza’ ya wanachama walio wabunge inayofanywa na baadhi ya vyama vya siasa.

Tendwa alisema hayo jana wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na matangazo yake kusikika jijini Dar es Salaam.

Alisema hulka iliyojitokeza hivi sasa kwa vyama vya siasa, hususan Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi, kuwafukuza uanachama wabunge kupitia vyama hivyo, haina tija kwa taifa.

Wakati NCCR-Mageuzi ilianza kwa kutangaza kumfukuza uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, CUF ilitangaza kumvua uanachama Mbunge wa Wawi kisiwani Pemba, Hamad Rashid Mohamed.

Wabunge hao walitangazwa kuvuliwa uanachama kwa nyakati tofauti wakiwa na baadhi ya wanachama waliosadikiwa kuwaunga mkono.

Hata hivyo, hatua za NCCR-Mageuzi na CUF zimepata upinzani kutoka kwa makundi mbalimbali ya kijamii na watu binafsi wanaoamini kuwa, vyama hivyo vilipaswa kutumia busara kufikia uamuzi huo.

Lakini viongozi wa vyama hivyo wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kuwa, kufukuzwa kwa wabunge hao kutoka NCCR-Mageuzi na CUF, kulifanyika kwa kufuata katiba zao.

Akizungumza na BBC jana, Tendwa alisema kama suala la kuwepo mgombea binafsi litashindikana katika kukabiliana na ‘fukuza fukuza’ hiyo, kuwepo utaratibu wa kubadili vifungu vya sheria husika, ili Mbunge anapofukuzwa uanachama aendelee kuwawakilisha wananchi wa jimbo lake la uchaguzi.

Alisema haiwezekani kwa mbunge aliyeshinda uchaguzi kwa njia ya kura, akafukuzwa uanachama kwenye kikao kilichoandaliwa kikiwa na ajenda moja pekee.

“Itakuwaje ajenda ya mkutano iwe moja peke yake, kumfukuza Kafulila (David, Mbunge wa Kigoma Kusini) ama Hamad Rashid (Mbunge wa Wawi) tu…hali hii inahitaji mabadiliko ili demokrasia iweze kukua,” alisema.

Alipohojiwa ikiwa azma ya kuwa na mgombea binafsi ama kumwezesha Mbunge kuendelea na uwakilishi baada ya kuvuliwa uanachama itawezekana kabla ya Katiba mpya, Tendwa alisema hilo linategemea busara ya mahakama.

Alisema pasipo kuingilia uhuru wa mahakama, kama uamuzi wa mashauri yaliyofikishwa kwenye mhimili huo yataamriwa kupitisha mgombea binafsi ama mbunge kuendelea kuwawakilisha wananchi hata anapofukuzwa uanachama, litakuwa suala la kufuta vifungu husika.

“Ikiwa mahakama itaamua hivyo, basi suala litakalobaki ni kufuta vifungu vya sheria zilizokuwa kikwazo hivyo kuyafanya maamuzi mengine kuwa batili,” alisema.

No comments:

Post a Comment