header

nmb

nmb

Wednesday, January 11, 2012

Tanesco yaja na teknolojia mpya ya LUKU

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), linatarajia kuanza kutumia teknolojia mpya na ya kisasa zaidi ya ukusanyaji ankara kwa watumiaji wa kati.

Meneja Uhusiano wa shirika hilo Badra Masoud (pichani), alisema jana katika taarifa yake kuwa lengo la kutumia teknolojia hiyo, ni kukabiliana na upotevu wa mapato.

“Shirika limefanikisha kupata teknolojia ya kisasa zaidi ya Automatic Meter Reader (AMR) ambayo itaanza kutumika mwaka huu,” alisema Masoud katika taarifa hiyo na kuongeza:

“Mita hizi mpya zitaunganisha teknolojia ya AMR na ile ya LUKU ambapo mteja atalipia umeme kabla ya kutumia na shirika litaweza kupata taarifa ya matumizi ya mteja pamoja na mwenendo wa mita kwa wakati. Hii itasaidia kuongeza mapato ya shirika na kudhibiti upotevu wa umeme.”

Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa, teknolojia hiyo ni ya kisasa na itasaidia kupunguza makosa ya kibinadamu, yaliyokuwa yakitokea wakati wa uandaaji wa ankara na usomaji wa mita.

Ilisema kuwa, teknolojia ya AMR inawezesha kusoma na kurekodi matumizi ya umeme kila saa kwa usahihi mkubwa.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa, mita za AMR hupeleka taarifa za usomaji wa mita kwenye kompyuta za shirika zilizopo makao makuu kila baada ya saa.

“Mfumo wa kompyuta za AMR hupokea na kuratibu taarifa za matumizi ya umeme kutoka kwenye mita ya mteja na kuandaa taarifa mbalimbali,” ilieleza taarifa hiyo:

“Mteja anayetumia mita za AMR anaweza kupata taarifa ya matumizi yake ya umeme wakati wowote anapohitaji taarifa hizo kwa kutumia tovuti ya Tanesco.”

No comments:

Post a Comment