header

nmb

nmb

Thursday, February 11, 2010

Aliye zua kizaazaa cha Mafisadi wa elimu huyuhapa

Bw. Msemakweli akionyesha kitabu alichokizindua kikiwa na picha za Baadhi ya Mawaziri watuumiwa kuhusu elimu zao
Mafisadi wa elimu 'waitwa' TCU
MAWAZIRI wanaodaiwa kughushi vyeti vya taaluma (mafisadi wa elimu) na wengine wanaotiliwa shaka wamepewa nafasi ya kuwasilisha vyeti vyao kwenye Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili kuthibitishwa na kuondoa utata katika jamii juu ya uhalali wa shahada zao, hasa walizozipata nje ya nchi.

Tamko hilo la (TCU) linakuja siku moja baada ya Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta kumtakasa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Dkt. David Mathayo kuwa elimu yake haina utata, hivyo watu waache kumzongazonga, lakini hakugusia vigogo wengine wanaodaiwa kuwa na vyeti feki au kusoma kwenye vyuo visivyotambulika.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Mayunga Nkunya alisema kuwasilisha vyeti TCU ndio njia itakayosaidia kuondoa minong'ono miongoni mwa jamii.

"Tume ingependa kusisitiza kuwa ili kuondoa utata katika jamii (juu) ya uhalali wa shahada za digrii alizonazo Mtanzania yeyote, hasa kutoka nje ya nchi, ni vizuri wahusika wakaleta vyeti vyao kwenye Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ili viweze kuthibitishwa uhalali wake na hivyo kuondoa minong'ono miongoni mwa jamii," alisema Profesa Nkunya.

Aliongeza kuwa iwapo TCU italetewa vyeti vyenye utata, itavifanyia tathmini kubaini uhalali wake au uhalali wa taaluma husika, kulingana na taratibu za kisheria zilizopo.


"Hata kama vyeti hivyo vingeletwa kwa kutathminiwa,utaratibu wa tume ni kuwafahamisha matokeo ya tathmini wahusika wenyewe binafsi au waajiri wao na sio kuwatoa taarifa zao kwenye vijitabu, vyombo vya habari au vinginevyo," alisema.

Alisema kuwa tume hiyo inalaani uchapishaji na usambazaji wa majina ya raia wa Tanzania kama alivyofanya Bw. Msemakweli na kusema kuwa vitendo hivyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu hivyo, hana ruhusa hiyo na ni vitendo vya ukiukwaji wa utawala wa sheria.

No comments:

Post a Comment