IMEELEZWA kuwa ukosefu wa uelewa juu ya makosa ya jinai huchangia kuongezeka kwa makosa ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia katika jamii.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania(TPF), SACP Elice Mapunda wakati akizindua mradi wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto jijini Dar es Salaam ulioshirikisha wadau mbalimbali kutoka serikalini, wanasheria, wanataaluma na asasi za kiraia .
“ Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kumekuwa na vitendo vingi vya makosa ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia katika jamii kutokana na sababu kuwa havitolewi taarifa ili wahusika wachukuliwe hatua,” alisema Mapunda.
Alisema watu wengi hawafahamu kuwa vitendo vya ubakaji , kupata ujauzito, kukatisha masomo, wizi, ujambazi na madawa ya kulevya vinavyofanywa na watoto ni chanzo cha ukatili wa kijinsia waliofanyiwa mama zao.
“Hivyo lengo la mradi huo ni kutoa elimu na mafunzo ya suala hilo kupitia vipeperushi na vitabu”.Aliongeza
Naye Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi, Robert Manumba, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa uzinduzi huo, alisema Bara la Afrika bado linaendelea kuathirika na mfumo dume ambao ukiendelea kuachiliwa inaweza kusababaisha uvunjifu wa amani.
“Mifumo hii ni hatari katika utengamano wa taifa,” alisema Manumba huku akisisitiza kwamba Watanzania wote wanahaki sawa, hivyo mapambano juu ya suala hilo si lelemama yanahitaji ushirikiano wa jamii nzima badala kuliachia jeshi hilo.
Aidha Manumba alizitaka taasisi mbalimbali kushiriki katika mapambano hayo kwa kukemea mila na desturi ambazo zinachangia vitendo hivyo.
Aliitaka jamii iungane na jeshi hilo kwa kuwa suala la uhalifu liko katika jamii.
Manumba aliongeza kuwa nguvu za pamoja kutoka kwa wadau mbalimbali katika kupambana na tatizo zitasaidia kupunguza masuala ya uhalifu.
Katika uzinduzi huo, Manumba alizindua vitabu viwili ambavyo ni “ukatili wa kijinsia ni kosa” na cha pili ni “sheria za ukatili wa kijinsia”.
No comments:
Post a Comment