header

nmb

nmb

Thursday, June 10, 2010

MAKALA YA MAKIRIKIRI,NA UJIO WAO.LEO WAKO MKOANI MBEYA!!



KATIKA sanaa ya muziki wa asili, ukuorodhesha majina matano kati ya hayo huwezi kulikosa jina la Makhirikhiri ambalo kwa sasa linazidi kujipatia umaarufu kila kukicha.
Kundi hili linaundwa na wasanii sita ikiwa ni wanaume wanne pamoja na wanawake wawili, ambao wanaimba kwa kutumia lugha ya Kiswana inayotumika katika nchi ya Botswana.
Kundi hilo lipo nchini kwa takribani wiki mbili likiwa katika ziara kwenye mikoa mbalimbali ambapo lilianzia kufanya onesho katika Mkoa wa Mwanza, likaenda Mkoani Shinyanga na baadaye lilitua Dar es Salaam na kufanya maonesho kadhaa na sasa lipo katika mikakati ya kufanya onesho la mwisho mkoani Mbeya ambapo litafanyika Juni 12 mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalum, Kiongozi wa kundi hilo, Moses Malapela 'Shumba Ratshega', anasema kuwa kundi lao lianazidi kujipatia umaarufu mkubwa barani Afrika kutokana na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujumbe wanaoutoa katika nyimbo zao.
Anasema kuwa wameshatambelea nchi mbalimbali za Afrika kwa ajili ya kutangaza Utamaduni wao ambapo pia wamepata mialiko mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya maonesho mbalimbali nchini Afrika Kusini katika Fainali za Kombe la Dunia.
Anasema kuwa yeye alianza kuimba muziki wa asili tangu akiwa mdogo ambapo mwaka 2006 aliachia albamu yake ya kwanza ya Masiela akiwa kama msanii wa kujitemea ambayo ilianza kumpandisha chati na kuamua kuunda kundi lake la Matsuwe Traditional Dance Group maarufu kama Makhirikhiri.
Anasema kuwa baada ya kupata mafanikio makubwa aliifanya kila jitihada ya kufanya shoo na kuimba ambapo wakaonekana kuwa tofauti na wasanii wengine wa muziki na kuwa maarufu zaidi ambapo mwaka 2007 walizindua albamu ya kundi inayoitwa Makhirikhiri ambayo ina jumla ya nyimbo kumi.
Anasema kuwa maana na jina Makhirikhiri ni udanganyifu wa mapenzi hasa kwa wanandoa ambayo husababisha ongezeko la maambukizi ya Ugonjwa wa ukimwi.
Amezitaja nyimbo ambazo zipo katika albamu yao kuwa ni pamoja na Dumelang, Masa, Sengwenengwene, Sananapo, Tsabana, Makhirikhiri, Bantalola, Mmaamotaj, Aids pamoja na Dikgafela.
Amewataja wasanii wanaounda kundi hilo kuwa ni Philip Simon, Linda Mosimanagare, Olebile Edson, Nametso Sebele na Motheo Johnson.
Anasema kuwa wameshafanya maonesho mbalimbali nchini Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini, China na Namibia ambapo sasa wana miliko katika nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Anasema kuwa ziara yao nchini Tanzania, imewafunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuelewa na kujifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pmaoja na Utamaduni.
Anasema kuwa wamependa mazingira ya Tanzania hivyo baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia wanatarajia kuja kufanya maonesho mbalimbali kwani wameona kuwa Tanzania pia kuna mashabiki wao wengi.
Anasema kuwa nyimbo zao nyingi wanatoa ujumbe unaohusu Ukimwi kutokana na nchi yao kuwa na wagonjwa wengi wa Ukimwi hivyo wanajitahidi kuimba nyimbo hizo ili kuweza kupunguza maambukizi.
Maonyesho ya kundi hilo nchini, yamedhaminiwa na Kampuni ya Business Times ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Majira, Spoti Starehe, Business Times, Dar Leo na pia wamiliki wa Kituo cha 100.5 Times FM pamoja na Kampuni ya Uchapishaji ya Business Printer, Tigo, Global Publishers, Aurora, Tai Five ya Mwanza pamoja na Giraffe Hotel.
"Tumefurahia sana ziara ya Tanzania ambapo pia tumejifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na Utamaduni wa Tanzania hivyo kwa kuwa ni mara yetu ya kwanza kuja hapa, tutafanya kila liwezekanalo turudi tena kwa ajili ya kufanya maonesho sehemu ambazo hatujafika" alisema Shumba Ratshega.
Ametoa wito kwa Serikali ya Tanzania kuvisaidia vikundi vya muziki wa asili nchini kwani ndio kielelezo kinachoweza kuitangaza nchi na Utamaduni wake katika Mataifa mbalimnbali.
Katika Uzinduzi wa onesho la kwanza lililofanyika Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Mgeni rasmi alitakiwa kuwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Joel Bendera lakini aliwakilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni, Herman Mwansoko.
Anasema kuwa ujio wa Makhirikhiri nchini, nifaraja kubwa kwa Watanzania ambapo wameweza kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa wasanii wa kundi hilo kupitia ujumbe uliopo katika nyimbo zao.
Anasema kuwa kwa hapa nchini, baadhi ya mtindo wanaotumia Makhirikhiri, unatumika sana katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania kama vile ngoma za Mganda, Lizombe,Kitoto na nyinginezo.
Anasema kuwa wasanii wa ngoma za asili wa Tanzania, hawana budi kuchukua mazuri yote wanayofanya Makhirikhiri na kuyazingatia ili kuweza kuendeleza na kukuza Utamaduni.
Anasema kuwa ngoma za Tanzania zinaweza kuwa kivutio kikubwa na zikauzika na wasanii wakajiongezea kipato kwa kutumia sanaa zao.
Mwandishi Victar5

No comments:

Post a Comment