header

nmb

nmb

Saturday, April 3, 2010

POLISI TZ WAONYA WAHUNI NA MADEREVA WANAO ENDESHA MAGARI KWA FURUJO WAKATI HUU WA PASAKA!!

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini A.Mpinga

Msemaji wa jeshi la polisi nchini A.Msika

JESHI la Polisi Tanzania limewataka abiria kuchukua hadhari ya kuepuka kupokea vyakula ama vinywaji kutoka kwa watu wasiowafahamu ili kuepuka kulishwa sumu na madawa ya kulevya kisha kuibiwa mali zao.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Bw. Abdulla Mssika alisema jana Dar es Salaam wazazi nao wachunge watoto na vijana wao katika matembezi wanapokwenda kuogolea kwenye fukwe za maziwa ama bahari pasipo uangalizi wa kutosha ili kuepuka kuzama au kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

"Makamanda wameagizwa kuhakikisha wanaweka ulinzi wa kutosha katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu na kufanya doria katika maeneo mbalimbali katika himaya zao ili kuhakikishia usalama wa wananchi na mali zao katika kipindi cha mapunziko ya muda mrefu ya Pasaka," alisema Mssika.

Wazazi wametakiwa kuchunga vijana wao kwenda kwenye mabanda ya video yaliyojaa kila mahali kuangalia picha zisizo na maadili kwani zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa mmonyoko wa maadili.

Bw. Mssika alisema polisi limewataka wazazi, walezi na viongozi wote wa Serikali za Mitaa, wamiliki wa nyumba za wageni, kumbi za starehe na wamiliki wa nyumba zenye vibanda vya video watoe ushirikiano kwa polisi kufichua maovu yanayofanyika.

Wakati huo huo Kikosi cha Usalama Barabarani kimetangaza kuwafutia leseni madereva wote watakaobainika na makosa ya barabarani pamoja na kupelekwa mahakamani.

Kamanda wa Kikosi cha Usalam Barabarani Tanzania Bw. Mohamed Mpinga alisema jana Dar es Salaam kuwa dereva atakayebainika na kosa kwa mara ya kwanza atatozwa faini ya Sh.
200,000 hadi Sh. 500,000 na leseni yake kugongwa muhuri atakaporudia kosa mara ya pili atafungiwa leseni yake.

Amewatahadharisha watumiaji wote wa barabara hasa madereva wa magari madogo, dala dala , pikipiki, baiskeli maguta, mikokoteni na wale waendao kwa miguu kujiepusha na vitendo vyovyote vitakavyoashiria kusababisha ajali.

"Kikosi chote cha askari wa usalama barabarani tutakuwa kazini kuhakikisha kuwa hakuna dereva atakayeendesha gari kwa uzembe ama kwa ulevi na kusababisha ajali za makusudi,"alisema Bw. Mpinga.

Alisema makondakta na mawakala wa mabasi wasiruhusu basi kujaa kupita uwezo wake na kwamba yeyote atakayekaidi na kukiuka maagizo hayo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kukamatwa na kufungiwa leseni yake na kufikishwa mahakamani.

Bw. Mpinga alisema askari wote wa kikosi cha usalama barabarani kwa kushirikiana na makachero wa polisi na wale wenye sare za kawaida watatawanywa katika maeneo mbali mbali kuhakikisha kuwa ajali za barabarani hasa katika kipindi hiki cha sikukuu zinakoma.

Aliwataka madereva wote wanaokodiwa na vijana kwenda kwenye kumbi za starehe kuwa makini na matumizi ya barabara na pia kuacha kupiga kelele barabarani pamoja na kuepuka kufunga vitambaa nyuma ya gari zao atakeyekamatwa atachukuliwa hatua za kisheria.

No comments:

Post a Comment