header

nmb

nmb

Saturday, April 3, 2010

MKUNGU WA NDIZI WAMPONZA DKT TEMEKE HOSPITALI!!




DAKTARI wa Hospitali ya Temeke, Dunstan Kabelwa amedai kukamatwa, kufungwa pingu na kisha kulipishwa faini ya sh. 118,000 na Ofisa Mtendaji Kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Same baada ya kuzuka mabishano ya kupitisha mikungu tisa ya ndizi.
Akizungumza katika ofisi za Majira jana, Dkt. Kabelwa alisema tukio hilo lilitokea Jumanne Machi 30 katika kuzuizi cha Wizara ya Mali Asili na Utalii cha Kihurio, Same mkoani Kilimanjaro akitokea Gonja kwa wazazi wake kwenda Dar es Salaam katika kituo chake cha kazi.

Walipofika katika kuzuizi hicho, mgambo mmoja aliyemtambua kwa jina la Tall alikagua gari lao kisha kumtaka mwenye mikungu ya ndizi amfuate kibanda cha walinzi ambako alimtaka alipe ushuru wa sh. 30,000 au akiwa hana fedha hizo atoe sh. 15,000 kwa ajili yake na ofisa Mtendaji wa Kata ya Kihurio.

"Baada ya kuingia ndani ya kibanda,mgambo akaniambia nilipe sh. 30,000 au sh. 15,000 ambazo zitakuwa za kwake na Mtendaji wa Kata ya Kihurio halafu tuendelee na safari yetu, mimi niligoma kutoa rushwa,"alidai Dkt.Kabelwa.

Dkt. Kabelwa alidai kuwa hakukubaliana na ushuru huo na mgambo huyo kumwita Ofisa Mtendaji wa Kata Bw. Yusuf Kivaju aliyemtaka asome tangazo ambalo linasomeka kuwa ushuru utalipwa kwa watakaobeba mazao ya biashara kwenye gunia lenye uzito wa zaidi ya kilo 100 hivyo ndizi mikungu tisa hazifiki hata kilo 20 ikipimwa kwa pamoja.

Alisema hapakuwa na uhalali wa kulipa fedha hizo, aliwagomea kukubaliana nao, kauli ambayo ilimkasirisha Mtendaji Kata Bw. Kivaju aliyetoa amri kufungwa pingu na kumpakia kwenye pikipiki hadi ofisi ya Kata ya Kihurio.

Dkt. Kabelwa alisema baada ya kufika ofisi ya Kata, Mtendaji huyo alimwacha na kudai amesahau funguo za pingu hivyo alifunga safari kurudi kuzichukua kipindi hicho mkono wa kulia uliokuwa umebanwa kwa pingu ulianza kuvimba.

Alisema baada ya muda Mtendaji Kata alirejea bila kuwa na funguo na kutafuta msumari na kuanza kukorokocha pingu na kufanikiwa kufungua mkono wa kushoto lakini wa kulia uligoma kufunguka.

Wakati daktari huyo akilalamika kuumia, mkono uliokuwa umevimba huku jitihada za kufungua pingu hizo kufanikiwa saa 11 jioni na kuamuriwa alipe sh. 118,000 ambazo alilazimika kuzitoa ili anusuru usalama wake na kuwahi kutibiwa mkono.

Alisema alipewa stakabadhi ya kwanza namba 0162621 ya sh. 50,000 ilikuwa ya adhabu ya kukataa kulipa ushuru,ya pili namba 0162622 iliyokuwa kwa jina la dereva wake Bw. Omari Ibrahim Omari alidaiwa ya kuvunja geti la ushuru na nyingine namba 0162623 ya ushuru wa ndizi.

Mkazi wa Kihurio Usambara, Bw. Said Baruti aliyeshuhudia tukio hilo alisema msaada wake wa kufungua pingu kutumia msumari ndio uliomuokoa daktari huyo asipate madhara ya kuvimba mkono.

"Mimi ni mgambo nimezitumia pingu muda mrefu, nina uzoefu nazo hivyo nilitoa msaada wa kumfungua daktari kutumia msumari kuokoa madhara makubwa ambayo yangetokea kutokana na mkono ulikuwa ukivimba kila saa zilivyosogea," alisema Bw. Baruti.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kihurio Bw. Kivaju alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo alijibu kwa njia ya simu ya mkononi kuwa faini aliyolipishwa Dkt. Kabelwa ya sh. 118,000 ilitokana na ubishi wa kutaka asilipie chochote.

Alisema Dkt. Kabelwa hakuwa muungwana na gari lake kulazimisha kutaka kuondoka ndio maana walichukua nguvu ya ziada ya kumfunga pingu na kumfikisha ofisi za Kata kwa hatua zaidi.

Alisema kushindwa kufunguka kwa pingu hizo kulitokana na shati la Dkt. Kabelwa kushikwa na reli za pingu hizo hivyo kulazimika kutumia njia nyingine kufungua.
"Sheria za Halmashauri ya Wilaya ya Same inasema ni kosa kwa mtu yoyote kukaidi kutii amri halali iliyotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Same kuhusu ushuru wa mazao, faini yake haipungui wala kuzidi sh. 50,000"alisema Bw. Kivaju.

Bw. Kivaju alipoulizwa daktari huyo alikuwa na mizigo mkubwa gani mpaka alipishwe ushuru wa sh. 118,000, alisema ni ndizi mikungu 30, mahindi magunia 50 na iliki magunia matatu ambavyo havikuorodheshwa kwenye risiti za malipo hayo.

Hata hivyo Dkt. Kabelwa alipinga vikali kuwa na idadi kubwa ya mizigo na kuongeza kuwa hiyo inawezekana kuwa kizuizi hicho kinawalipisha ushuru watu ambao mizigo yao si ya kibiashara na hawana sehemu ya kulalamika kujua haki zao.

No comments:

Post a Comment