Itono, Ukonga
WAKAZI wa Ukonga Mtaa wa Madafu wametakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuweza kudhibiti wizi mpya ulioibuka ambapo wanawake hujifanya ombaomba kisha kuiba mali za watu.
Wakizungumza , baadhi ya wakazi wa mtaa huo wamesema kuwa tabia hiyo imejitokeza zaidi ya miezi mitatu sasa ambapo kuna baadhi ya wanawake wamekuwa wakijifanya kupita mitaani na kuomba msaada wa maji ya kunywa au kitu chochote ili kupata mwanya wa kuiba mali za watu, zikiwamo simu za mkononi.
Amina Ally, mkazi wa Ukonga, ameliambia gazeti hili kuwa wanawake hao wamekuwa na tabia ya kubeba watoto mgongoni na kujifanya wanaomba maji ya kunywa, baada ya hapo huiba chochote kilichopo.
Wamesema kesi za aina hii zimekuwa zikifikishwa katika vituo vya polisi vilivyopo jirani yao ili kuweza kushughulikiwa lakini hawaoni kinachoendelea na hatimaye kuona tabia hii ikiongezeka.
Wameliomba jeshi la polisi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakazi wa mitaa hiyo ili kuweza kuikomesha tabia hiyo na kuhakikisha mali za wananchi zinakuwa salama.
Naye Juma Shaban mkazi wa eneo hilo amewataka wananchi kushirikiana ili kuhakikisha tabia hiyo inakomeshwa kwani kuwaachia wanawake peke yao kutawaongezea mzigo.
Amesema wananchi kuwa makini na wageni wanaofika majumbani mwao ambao hawawafahamu.
No comments:
Post a Comment