header

nmb

nmb

Saturday, July 23, 2016

WASIFU WA DK. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI


MGOMBEA NAFASI YA MWENYEKITI WA CCM

1.0.  MAISHA YAKE

Ndugu John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa Oktoba 29, mwaka 1959 katika kijiji cha Chato, Wilayani Biharamulo katika Mkoa wa Kagera. Hivi sasa Chato ni Wilaya katika Mkoa wa Geita. Ndugu Magufuli ni Daktari wa Falsafa (PhD) ya Kemia. Ana mke  na watoto saba.  Alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba, 2015 kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (C.C.M). Aliapishwa na kuanza rasmi majukumu yake ya kuiongoza Tanzania tarehe 5 Novemba, 2015.

Tangu ameingia madarakani, Rais Dkt. Magufuli, ameonesha kuwa ana sifa zote muhimu za uongozi. Ana dira, maono na malengo kuhusu anakotaka Taifa liende. Ana mikakati ya kutekeleza dira na maono yake. Haogopi kufanya maamuzi makini. Ana kiu ya kuona Taifa linapata maendeleo. Amejipambanua kuwa yeye ni mtetezi wa wanyonge na dhamira yake kubwa ni kuona wananchi wanapata huduma bora  za jamii na kero zao zinaondoka.

2.0.  ELIMU NA MAFUNZO

Rais Dkt. Magufuli alianza elimu ya msingi katika Shule ya msingi Chato mwaka 1967 na kumaliza mwaka 1974. Mwaka 1975 alianza masomo ya sekondari katika Shule ya Seminari ya Katoke Mkoani Kagera.  Mwaka 1977 alihamia shule ya sekondari ya Lake iliyopo Mkoani Mwanza  na kuhitimu kidato cha Nne mwaka 1978. Kuanzia mwaka 1979 hadi 1981 alifanya masomo ya kidato cha Tano na  Sita katika shule ya Sekondari ya Mkwawa Mkoa wa Iringa  .

Mwaka 1981 hadi 1982 alisoma Chuo cha Ualimu Mkwawa na kuhitimu Stashahada ya Ualimu ya Masomo ya Kemia na Hisabati.  Mwezi Julai hadi Disemba mwaka 1983, Dkt. Magufuli alipata mafunzo ya kijeshi  katika Jeshi la  kujenga Taifa kikosi cha Makutupora mkoa wa Dodoma. Mwezi Januari hadi Machi 1984 alihamishiwa kikosi cha mafunzo Jeshi la Kujenga Taifa Makuyuni, Arusha.  Mwezi huo wa Machi alihamia kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa Mpwapwa Dodoma na kumaliza mafunzo mwezi Juni 1984.

Mwaka 1985 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kusoma Shahada ya kwanza ya Sayansi na Ualimu akijikita katika masomo ya Kemia na Hisabati. Alitunukiwa Shahada hiyo mwaka 1988.  Mwaka 1991 hadi 1994 alisoma na kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika fani ya Kemia iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Chuo Kikuu cha Salford cha Uingereza. Mwaka 2006 alijiunga na  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya Shahada ya Uzamivu katika Fani ya Kemia na kufanikiwa kuhitimu mwaka 2009.

3.0.  UZOEFU WA NDANI YA  SERIKALI

Baada ya kuhitimu masomo yake ya Stashahada ya Ualimu, mwaka 1982 hadi 1983 Dkt. Magufuli alikuwa Mwalimu katika shule ya Sekondari ya Sengerema iliyopo Mkoani Mwanza akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati.  Mwaka 1989 alijiunga na Chama Cha Ushirika cha Nyanza Mkoani Mwanza, ambapo alifanya kazi kama Mkemia Mkuu  hadi mwaka  1995.

Mwaka 1995 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki Mkoa wa Kagera.  Baada ya Uchaguzi, Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi nafasi ambayo aliitumikia  hadi mwaka 2000.  Mwaka 2000 alichaguliwa kwa mara ya pili kuwa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki lakini mara hii akipita bila kupingwa.  Mwaka huo huo aliteuliwa kuwa Waziri kamili wa Wizara ya Ujenzi hadi mwaka 2005. 

Mwaka 2005 Rais Dkt. Magufuli alichaguliwa kwa mara ya tatu kuwa mbunge wa jimbo la Biharamulo Mashariki, kwa mara nyingine akipita bila kupingwa.   Baada ya uchaguzi, Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2008 ambapo alihamishiwa Wizara ya   Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi hadi hadi mwaka 2010.

Mwaka 2010 Dkt. Magufuli alichaguliwa kwa mara ya nne  kuwa  Mbunge lakini, kufuatia mgawanyo wa majimbo uliofanyika, mara hii katika Jimbo jipya la Chato.  Baada ya uchaguzi, aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015.

Wakati akiwa Mbunge na Waziri, Dkt. Magufuli amefanya shughuli na kushika nyadhifa kadhaa ndani na nje ya nchi. Mwaka 2014, Dkt. Magufuli alishiriki katika Bunge Maalum la Kutunga Katiba Mpya akiwa  ni Mjumbe wa Bunge hilo. Aidha, wakati akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliweza kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza (Co-Chair) wa Mkutano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN-Habitat).

Tarehe 25 Oktoba, 2015 Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tarehe 5 Novemba, 2015 aliapishwa kushika rasmi wadhifa huo.


4.0.  UZOEFU WA UONGOZI NDANI YA CHAMA

Rais Dkt. Magufuli alijiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977. Amekuwa Mwanachama mwaminifu na ameshika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama. Nafasi alizowahi kushika ni pamoja na kuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa. 

Sambamba na kushika nafasi mbalimbali za uongozi, Dkt. Magufuli mara zote alijitoa kukitetea Chama na kuhakikisha kinapata ushindi. Alishiriki kikamilifu kuwafanyia kampeni wagombea wa CCM katika Chaguzi Ndogo zilizofayika katika majimbo ya Busanda, Biharamulo Magharibi na Igunga na kupata ushindi.  Katika Mkutano Mkuu wa CCM wa tarehe 11 – 12 Novemba mwaka 2012, Dkt. Magufuli alikuwa miongoni mwa Mawaziri wachache waliopata fursa ya kuelezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama ya Mwaka 2010 – 2015. Alielezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani, hususan katika sekta ya miundombinu.

Tarehe 11 mwezi Julai, 2015 Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ulimchagua na kumteua Dkt. Magufuli kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Aliinadi vyema Ilani ya uchaguzi ya CCM (2015) na kukiwezesha Chama kupata ushindi mkubwa. Tarehe 25 Oktoba, 2015 alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Nafasi hiyo imemwezesha kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.

5.0.  UFANISI KATIKA UONGOZI

Dkt. Magufuli ni kiongozi mnyenyekevu, aliye na hofu ya Mungu, mkweli, mtekelezaji wa ahadi, mwadilifu, shupavu, mahiri, mbunifu, mtafiti, mchapakazi na mtetezi wa wanyonge. Ni kiongozi mpenda haki na mchukia dhuluma, rushwa, ufisadi na ubaguzi wa aina yoyote ile.  Ni kiongozi mwenye msimamo na mtetezi wa yale anayoyaamini. 

Katika nyadhifa zote alizopata kutumikia alifanya kazi kwa uadilifu na umahiri mkubwa. Amejidhihirisha na kujipambanua kuwa ni mfuatiliaji na msimamizi wa sheria. Akiwa Mwalimu Sengerema Sekondari aliwezesha wanafunzi wote wa darasa lake kufaulu masomo ya Hesabu na Kemia aliyokuwa akiyafundisha. Akiwa Mkemia Mkuu wa Chama cha Ushirika cha Nyanza alisimamia vyema ubora wa uzalishaji wa mafuta ya Pamba na kuifanya Kampuni ya Nyanza kuwa mzalishaji mzuri wa mafuta ya Pamba. 

Akiwa Waziri wa Ujenzi anakumbukwa kwa kubuni na kusanifu miradi ya ujenzi wa barabara, kusimamia vizuri matumizi ya fedha na kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango na kwa wakati uliopangwa. Uwezo wake katika kubuni na kusanifu miradi ya barabara uliigwa na nchi majirani, ikiwemo Kenya. Ameondoka Wizara ya Ujenzi akiwa amesimamia ujenzi wa zaidi ya Kilometa 17,000 za barabara za lami, madaraja makubwa zaidi ya 14 na madaraja madogo madogo zaidi ya 7,000 na vivuko. Aidha, alisimamia vizuri taasisi mbalimbali za Makandarasi, Wahandisi, Wabunifu na Wakadiriaji Majengo.

Dkt. Magufuli pia anasifika kwa uwezo wake mkubwa wa kuweka kumbukumbu ya kazi zake.  Akiwa Wizara ya Ujenzi aliweza kutaja majina ya barabara zilizojengwa au zilizokuwa katika hatua za ujenzi, urefu wake, majina ya wakandarasi pamoja na gharama za ujenzi bila kusoma mahali popote.  Wakati wa Rais Mstaafu Benjamini William Mkapa alimwita “Askari wa Mwavuli”.  

Akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisimamia upimaji wa ardhi za vijiji na viwanja vya makazi, na kushughulikia migogoro mingi ya ardhi iliyowahusu wananchi wa maisha ya chini. Wakati  akiwa Waziri wa Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi alikuwa maarufu wa kutambua na kutaja idadi ya mifugo,  kama vile samaki,  ngómbe, mbuzi, kondoo, kuku, mbwa n.k. Kitendo cha kukamata meli ya kichina iliyokuwa ikivua samaki kwa wizi ndani ya Bahari Kuu ya Hindi eneo la Tanzania kilidhihirisha uzalendo kwa Taifa lake.  Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Kikwete alimpachika jina maarufu la “Tingatinga”. 

Sifa hizi nzuri ameendelea nazo hata baada ya kuchaguliwa kuwa Rais. Katika miezi michache ya uongozi wake amethibitisha anatekeleza ahadi. Aliahidi kutoa elimu bila malipo na kuanzisha Mahakama ya Mafisadi. Ameweza kusimamia nidhamu kwenye utumishi wa umma kwa kuondoa watumishi hewa na kuchukua hatua dhidi ya watumishi wa umma wasio waaminifu, wala rushwa, wazembe na wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Ameweza kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Kwa hakika Dkt. Magufuli anaakisi uongozi bora unaopaswa kuigwa na viongozi wengi Barani Afrika na Dunia.

6.0. DHIMA YA UONGOZI WA SERIKALI YA AWAMU YA TANO 2015 – 2020) NA MALENGO YAKE MAHSUSI

Ilani ya uchaguzi ya CCM  ya Mwaka 2015 – 2020 inazielekeza serikali zake kutumia nguvu zake zote kuendelea kupambana na changamoto kubwa nne;- Kwanza kuondoa umaskini, Pili, kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, Tatu, kuendeleza vita dhidi ya adui rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, na Nne, kuendelea kudumisha amani, ulinzi na usalama wa maisha ya Watanzania na mali zao.

Sambamba na kutekeleza mambo hayo makubwa manne, kipindi cha Kampeni na wakati akizindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba, 2015 Rais Dkt. Magufuli alitaja malengo mahsusi ya Serikali ya Awamu ya Tano. Malengo hayo ni haya yafuatayo:

·    Kudumisha Muungano, Amani na Umoja wa Tanzania. Serikali haitamwonea aibu mtu mwenye nia ya kuvunja Muungano na kuvuruga amani na mshikamano katika nchi. Hili alilidhihirisha vizuri wakati wa uchaguzi wa marudio huko Zanzibar, kwani Uchaguzi ulifanyika kwa amani na utulivu.

·    Kujenga Uchumi wa Viwanda ili kufikia azma ya kuwa nchi ya  uchumi wa kati kulingana na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.  Viwanda vinalengwa ni vyenye kutumia nguvu kazi kubwa, malighafi za ndani ya nchi, kuzalisha bidhaa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi. Nia ni kukabiliana na tatizo la ajira na umasikini;

·     Kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi, hususan miundombinu ya usafiri na nishati;

·     Kuimarisha huduma za jamii, hususan elimu, Afya na Maji. Lengo ni kuhakikisha huduma hizo zinapatakana sio tu kwa urahisi bali pia kwa ubora unaostahili ili kukabiliana na maadui ujinga, umaskini na maradhi;

·     Kusimamia uwajibikaji wa utumishi wa umma na kuondoa urasimu ndani ya Serikali. Lengo ni kuhakikisha watumishi wa umma wanafanya kazi kwa ueledi, uadilifu na kujituma ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati;

·      Kuimarisha usimamizi wa rasilimali za nchi, ikiwemo kuhifadhi mazingira na kuzidisha vita dhidi ya ujangili. Lengo ni kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha watu wote wa kizazi cha sasa na kijacho. Aidha, ukusanyaji wa mapato ya Serikali na udhibiti wa matumizi ya Serikali nao utaimarishwa;

·      Kusimamia utawala bora unaozingatia sheria na haki za binadamu. Jitihada za makusudi zitaelekezwa katika kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, dhuluma na uonevu wa aina yoyote. Aidha, maslahi ya makundi mbalimbali katika jamii, ikiwemo wanawake, wazee, watu wenye ulemavu na watoto yatalindwa. Kwa upande mwingine, wananchi watahimizwa kuheshimu na kufuata sheria za nchi;

·       Kulinda usalama wa raia na mali zao kwa kupambana na uhalifu, ikiwemo wizi, ujambazi, tatizo la dawa za kulevya n.k.

·       Kudumisha na kuendeleza ujirani mwema, mahusiano mema na Mataifa mengine duniani pamoja na Mashirika ya Kimataifa na Kikanda;

·       Kuendeleza na kusimamia vizuri shughuli za michezo, sanaa, burudani na utamaduni, ikiwemo kukuza lugha ya Kiswahili.

HITIMISHO
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imedhamiria kuongeza kasi ya ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na kuwataka watanzania  washiriki kufanya kazi kwa bidii na maarifa  ndani ya falsafa ya HAPA KAZI TU. Dhamira hii inakusudia kuwezesha Taifa letu kufikia Uchumi wa Kati uaoongozwa na Viwanda ili kutimiza malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.

No comments:

Post a Comment