Moja ya gari ambayo lilikuwa linabeba kokoto shuleni hapo
Wazazi wa watoto
wanaosoma shule ya msingi Lubwe iliyopo kitongoji cha Lubwe Kijiji cha
Kikota Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya wamemtaka Mwalimu
mkuu wa shule hiyo Karim Msisiri kuondolewa shuleni hapo kwa tuhuma za
kufuja raslimali za shule.
Kauli hiyo wameitoa
katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho ulioitishwa na
Mratibu wa elimu Kata Bi Tujengwe Mwangobola na kusimamiwa na
Mwenyekiti wa kijiji Godwin Mwakasege ambapo Mratibu Kata ya Ilundo Hard
Mwambula alialikwa kusikiliza.
Wazazi walimtuhumu
mwalimu Msisiri kufuja zaidi ya shilingi laki tano zilizotokana na mauzo
ya mchanga na miti ambazo ni raslimali za kijiji zilizotolewa na kijiji
kwa ajili ya kuendeleza shule hiyo lakini amekuwa akizitumia kwa
matumizi binafsi huku shule ikikosa madirisha na sakafu katika madarasa.
Akiongea kwa niaba ya
kamati ya shule hiyo mjumbe Frank Mwangomo kutokana na vitendo vya
Mwalimu mkuu kukithiri na kutoshirikisha kamati imepelekea Mwenyekiti wa
kamati ya shule Edward Kabuka kujiuzuru.
Frank amesema kuwa
kamati ya shule hiyo pia imesikitishwa na kitendo cha Mwalimu huyo
kumtumia Mwenyekiti wa kamati ya awali aliyeenguliwa ambapo mwenyekiti
huyo alitafuna pesa za shule shilingi mia moja hamsini elfu,baada ya
kubanwa na mtendaji wa kijiji Felix Michael amerejesha shilingi elfu
themanini na kiasi kilichosalia kuahidi kurejesha Februari 27 mwaka huu.
Kwa upande wake
mwalimu mkuu amekiri kufanya makosa hayo na kuomba msamaha kutokana na
majukumu mengi na kuahidi kuwa hatarudia kufanya makosa tena hivyo
wazazi wasife moyo bali waendelee kushirikiana ili kukuza taaluma kwa
watoto wa shule hiyo.
Aidha mwalimu aliwaambia wazazi
kuwa kwa muda wa miezi saba amekusanya kiasi cha shilingi mia moja
hamsini na tisa elfu ambazo alikusanya kutokana na mauzo ya mchanga na
miti na fedha hizo zilikatiwa stakabadhi.
Baada ya mvutano mrefu Mratibu wa
Elimu aliwataka wazazi kupiga kura kujua hatima ya mwalimu kama abaki
shuleni au la,ndipo wazai waliotaka mwalimu asamehewe walikuwa 14 na
waliotaka mwalimu aondolewe walikuwa 30.
Kwa upande wake
Mratibu aliwaambia wazazi kuwa anaheshimu mawazo yao lakini hana mamlaka
ya kumwondoa mwalimu bali atapeleka mawazo yao kwa Afisa Elimu Wilaya
yeye ndiye ana uwezo wa kutoa maamuzi lakini aliwapa muda kama
watabatilisha uamuzi wao watoe taarifa kabla ya Februari 19 mwaka huu
katika mkutano watakaoitisha kupitia kwa mwenyekiti wa kijiji.
Wakati huo huo
uchunguzi umebaini mlinzi wa shule hiyo Hamisi Mbange anadai mshahara
wake kwa kipindi mwa mwaka 2012/2013 jumla ya shilingi laki tatu na elfu
ishirini na tano ambazo hajalipwa na uongozi wa shule kwa muda mrefu
bila mafanikio licha ya wazazi kuchangia shilingi elfu moja mia mbili
kwa mwaka kila mtoto.
Na Ezekiel Kamanga
Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment