WAANDAAJI wa Tamasha la Krismas wametangaza kuwa tamasha hilo litafanyika
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Desemba 25 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya
habari leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama
ilieleza kuwa awali mikoa sita iliomba kuwa mwenyeji wa tamasha hilo, lakini
kamati yake imeteua Mkoa wa Dar es Salaam uwe wa kwanza. “Kamati ya
Maandalizi ya Tamasha la Krismas imeamua lifanyike Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, halafu Desemba 26 tutatizama mkoa mwingine. Tunaomba mashabiki wetu
waendelee kutuunga mkono,” alisema Msama.
Alisema awali walipokea maombi kutoka
kwa wadau mbalimbali wa muziki wa Injili nchini wakiomba lifanyike katika mikoa
yao, ambayo ilikuwa ni Mbeya, Mwanza, Arusha, Dodoma, Dar es Salaam na Shinyanga.
Tamasha la Krismas linaandaliwa na Kampuni ya Msama
Promotion ya jijini Dar es Salaam, ambayo pia huandaa Tamasha la Pasaka kila
mwaka. Kwa mujibu wa Msama wanataka Tamasha la Krismas liwe bora zaidi
kuliko la Pasaka kwa kualika wasanii maarufu kutoka nje na ndani ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment