HATIMAYE Tanzania imewekwa kando rasmi
na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), katika kuunda
Shirikisho la Kisiasa litakaloziongoza nchi hizo.
Tayari marais wa nchi hizo, Paul Kagame
wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Pierre
Nkurunzinza wa Burundi wamekwishafikia makubaliano ya kuanzisha mchakato
wa kuandikwa kwa Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la nchi
wanachama wa EAC, bila kuishirikisha Tanzania.
Waziri wa Serikali za Mitaa wa Rwanda,
James Musoni, amekaririwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo akieleza
kuwa makubaliano ya kuanzishwa kwa mchakato wa kuandikwa kwa Rasimu ya
Katiba ya Shirikisho la Afrika Mashariki, yalifikiwa Septemba 12 mwaka
huu, mjini Kampala na marais wa Rwanda, Kenya na Uganda na hivi karibuni
Rais wa Burundi ambaye alialikwa katika mkutano huo na kushindwa
kuhudhuria, naye sasa amethibitisha ushirika wake katika shirikisho hilo
jipya.
Gazeti la The Sunday Times la Rwanda,
limemnukuu Waziri Musoni kuwa marais wa nchi hizo wamekubaliana
kukamilisha rasimu hiyo ndani ya muda mfupi.
Musoni ambaye alikiri kushiriki katika
mkutano wa marais hao ulioshirikisha pia maofisa waandamizi wa nchi hizo
isipokuwa Tanzania, alisema uamuzi uliofikiwa katika mkutano huo ambao
ni wa pili kufanyika, ni moja ya maagizo ya uamuzi uliofikiwa kwenye
mkutano wa kwanza uliofanyika pia mjini Kampala.
“Tumekubaliana juu ya kanuni za kisheria
na mpango mzima utakaotuongoza ili kupata Rasimu ya Katiba
itakayoliongoza shirikisho hilo la kisiasa,” alikaririwa Musoni.
Alieleza kuundwa kwa kikosi kazi maalumu
kitakachojulikana kwa jina la High Level Task Force (HLTF), ambacho
kitajumuisha wataalamu wa nyanja mbalimbali watakaoandika Rasimu hiyo
kwa namna ile ile ya ulivyoandaliwa mpango wa Itifaki ya soko la pamoja
la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Musoni alisema mawaziri wa nchi
wanachama waliopangiwa kushughulikia shirikisho hilo, wanatarajiwa
kuelezea mwelekeo wa mafanikio ya mpango huo katika mkutano mwingine
uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba huko Kigali Rwanda.
Kwa mara ya kwanza, marais Kagame,
Museveni na Kenyatta walikutana kufikia makubaliano ya kuharakisha
uundwaji wa shirikisho la kisiasa kwa nchi zao kwa kuondoa vikwazo vya
kiuchumi na kuweka hati ya vitambulisho vya pamoja na ushirikiano wa
kibiashara sambamba na kuzindua mradi wa ujenzi wa gati ya Bandari ya
Mombasa.
No comments:
Post a Comment