Makamu wa Rais Dkt. Mohamed Ghalib Bilal amesema serikali inafanya jitihada za kipekee kuhakikisha madini ya makaa ya mawe yanachimbwa na kuzalisha ili yaweze kuondoa kero ya tatizo la umeme nchini.
Ametoa kauli hiyo hivi karibuni alipotembelea mradi wa makaa ya mawe wa Ngaka uliopo kijiji cha Ngaka wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma na kuongeza kuwa nchi yetu itafaidika na uwepo wa rasilimali hii katika kuzalisha umeme wa uhakika.
Makamu wa Rais aliongeza kusema kuwa nchi ina uwezekano mkubwa wa kuzalisha umeme kwa miaka zaidi ya mia mbili kutokana na wingi wa makaa ya mawe yaliyopo mikoa ya Ruvuma,Iringa na Mbeya.
“Makaa haya ni hazina kubwa kwa taifa na ni kazi yetu kujipanga kuzalisha umeme hivyo nawasihi tukae mkoa wa kula kwani umeme utakuwa wa uhakika”alisema Makamu wa Rais.
Aidha alisema ni lazima tuhakikishe TANCOAL wanafanya kazi yao kikamilifu kwa kupatiwa ushirikiano stahili ili lengo la kuzalisha megawati 120 za umeme kwa mkoa wa Ruvuma kama walivyoweka lengo litimie
Kwa sasa mkoa wa Ruvuma unapata umeme unaozalishwa na majeneta katika wilaya za Mbinga,Songea na Tunduru ambapo kwa wilaya ya Namtumbo hadi sas hakuna umeme lakini kwa jitihada za serikali kufikia Juni mwaka huu umeme utapatikana.
Aliongeza kusema katika kutekeleza dira ya Taifa ya Taifa ya 2025 Tanzania itazalisha umeme wa makaa ya mawe yapo kwa wingi katika mkoa wa Ruvuma hivyo ni wajibu wetu kama Taifa kunufaika na madini yetu
“Nimesikia mengi yakisemwa kuhusu makaa ya mawe hivyo nikaamua kuja na kujionea mwenyewe hali ilivyo katika mgodi huu na niwahakikishie kuwa serikali itafanya kila liwezekalo kuona madini haya yanatumika kuzalisha umeme ili kero ya umeme wa dharura iondoke” alisisitiza Makamu wa Rais.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo Mkurugenzi wa shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Gideon Nasali alimweleza Makamu wa Rais kuwa hatua za kuipata kibali inachukua muda mrefu na hivyo kuomba nguvu za serikali kuondoa vikwazo ili kampuni TANCOAL ipatiwe leseni na kutekeleza mpango wake wa kuzalisha umeme wenye megawati 400.
Makamu wa Rais amewahakikishia wawekezaji hao kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha dhamira hii njema ya kuzalisha umeme kwa Taifa inafanikiwa na kuwaondolea wananchi kero ya upatikanaji wa umeme.
Kampuni ya TANCOAL imejipanga kuzalisha umeme utokanao na makaa ya mawe kwa kiwango cha megawati 400 ambapo watajenga njia ya kusafirisha umeme kutoka mgodini hadi Songea kisha TANESCO watengeneze njia ya kusafirisha umeme huo hadi Makambako na kuunganisha na gridi ya Taifa.
Alisema na kuongeza kuwa utakapo zalishwa umeme wa makaa ya mawe ambao ni wa uhakika utachangia kukuza uchumi wa Taifa kwani viwanda vingi vitanufaika na umeme huo hivyo kuinua uzalishaji na kuongeza thamani katika mazao ya wakulima.
Kwa sasa makaa ya mawe yanayozalishwa katika mgodi wa Ngaka yanatumika na viwanda vya saruji vya Mbeya na Tanga na pia madini husika yanauzwa kwa nchi ya Malawi.
Katika mradi huo serikali kupitia NDC inamiliki asilimia 30 na kampuni ya Intra Energy ya Singapole ina hisa 70 na utakaoanza uzailishaji utotoa fursa ya kuungana na mataifa mengi Duniani kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe.
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma
No comments:
Post a Comment