header

nmb

nmb

Tuesday, January 3, 2012

Dkt. J. K. Aiagiza aina ya Palahala TAWIRI kutafiti sababu za kutoweka kwa Mnyama

















Rais, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ameiagiza taasisi ya utafiti wa wanyamapori (Tanzania Wildlife Research Institute - TAWIRI-) kutafiti sababu za kutoweka kwa mnyama aina ya Palahala (Roosevelt Sable Antelope) katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani mkoani pwani na maeneo mengine walikokuwa wakionekana kwa wingi hapo awali.

Rais Kikwete ametoa agizo hilo mwanzoni mwa wiki kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI Dkt. Simon Mduma, baada ya kupokea maelezo ya Mpango wa Kitaifa wa Kuhifadhi Tembo nchini (Tanzania Elephant Management Plan), alipokutana na uongozi wa taasisi hiyo katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.

Mpango huo umeainisha vipaumbele vinavyohitaji kutiliwa maanani katika kuhifadhi na kudhibiti Tembo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Rais aliiagiza TAWIRI kwamba pamoja na kupata chanzo cha kutoweka kwa wanyama hao, pia itafutwe njia ya kuwarejesha tena, akisisitiza kwamba Palahala ni mnyama anayevutia sana na anaweza akawa kivutio cha ziada katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani, hasa kwa utalii wa upigaji picha.

Palahala ni mnyama anayevutia sana kutokana na umbo lake ambapo wawindaji hupendelea sana kumuwinda ili kupata pembe zake ndefu ambazo hutumika kama mapambo katika nyumba. Pembe hizo pia hutumika kuchezea ngoma za kiasili.

Rais Kikwete pia ameagiza kufanyike uchunguzi wa kina ili kujua sababu zilizosababisha kupungua kwa kasi kwa idadi ya tembo katika ukanda wa mbuga za wanyama za Selous na Mikumi, baada ya kustushwa na ripoti inayoonyesha kwamba zaidi ya tembo 30,000 wametoweka katika kipindi kifupi.

Rais alitoa agizo hilo baada ya Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI. Simon Mduma kutoa takwimu zilizoonyesha kwamba katika mbuga za Selous na Mikumi mwaka 2006 kulikuwa na tembo 74,900, na sensa iliyofanyika mwaka 2009 ilionyesha wamesalia 43,552.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.


No comments:

Post a Comment