Kiongozi wa upinzani nchini Malaysia, Anwar Ibrahim ameondolewa makosa ya ulawiti katika kesi iliyochukua karibu miaka miwili. Mwanasiasa huyo alituhumiwa kufanya ngono na aliyekuwa msaidizi wake wa kiume.
Hata hivyo jaji wa mahakama hiyo alisema uchunguzi wa DNA haukutoa ushahidi wowote.
Punde baada ya mahakama kutangaza uwamuzi huo, jamaa wa bw Anwar walionekana kububujikwa na machozi ya furaha huku wafuasi wake wakishangilia uwamuzi huo.
Wafuasi wa mwanasiasa huyo waliokusanyika nje ya mahakama mjini Kuala Lumpar wamekuwa wakisisitiza kwamba kesi hiyo haikufaa kufunguliwa tangu kuwasilishwa kwa tuhuma za ulawiti.
Hii ni mara ya pili bw. Anwar ameshtakiwa kwa kufanya ulawiti. Kesi dhidi yake zimepelekea kuwepo na msisimuko mkubwa wa kisiasa nchini Malaysia kwa zaidi ya muongo mmoja.
Anwar Ibrahim ametaja kesi hiyo kama iliyochochewa kisiasa japo serikali imekanusha kuhusika kwa vyovyote.
Huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa karibuni, chama tawala ambacho kimekuwa madarakani kwa zaidi ya nusu karne kinakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mrengo wa upinzani unaoongozwa na bw. Anwar.
No comments:
Post a Comment