header

nmb

nmb

Friday, June 11, 2010

RPC MBEYA ADAI ALIYEMTAJA KAUWAWA SI YEYE!!

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mbeya,Advocate Nyombi amesahihisha taarifa yake aliyoitoa juzi katika vyombo vya habari kuhusu kuuawa kwa watuhumiwa watatu wa ujambazi kati ya watano wakati wa kurushiana risasi katika Kijiji cha Nditu wilayani Rungwe,barabara ya Katumba,Mwakaleli wiki iliyopita ambapo watuhumiwa wawili walidaiwa kuingia mitini,kwamba mtuhumiwa Barick Martin(30),Mkazi wa Rufilyo,wilayani humo yupo hai na alitajwa kimakosa kuhusika katika tukio hilo na kuuawa. Nyombi alisema kuwa jina hilo lilitajwa kimakosa na wananchi waliofika katika eneo la tukio Juni 4, kwa ajili ya kuwatambua majambazi watatu waliouawa kwa kupiga risasi na polisi ambapo baadaye polisi walibaini kuwa aliyeuawa si Barick bali ni Bernad Anyosisye(32), mkazi wa Nzovwe,jijini Mbeya na kwamba waligundua hilo baada ya maiti yake kufikishwa Hospitali ya Rufaa Mbeya na ndugu kufika na kuichukua kwa ajili ya mazishi.
Katika tukio hilo la wiki iliyopita,Nyombi alivithibitishia vyombo vya habari kuwa Barick aliwahi kufungwa miaka mitatu jela na kuachiwa April 26, mwaka huu, ambapo alhamisi iliyopita,alikaririwa akisema kuwa majambazi hayo yaliuawa Juni 3, mwaka huu majira ya usiku.
Kamanda Nyombi alikaririwa akisema kuwa polisi walipokuwa katika doria yalifanikiwa kuyanasa majambazi hayo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa yalikuwa yakiwavizia wafanyabiashara wa mbao katika Barabara ya Katumba kijijini hapo. Aidha Kamanda Nyombi aliwataja majambazi waliouawa katika tukio lililotokea wilayani Rungwe waliotambuliwa kuwa ni Maneno Mtasiwa(30) Mkazi wa Block Q jijini hapa na Mfanyabiashara wa Viatu vya Mitumba katika Soko la Mwanjelwa, Zawadi Pamelo (32) na Mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Benny Makazi wa Nzovwe jijini hapa. Hata Hivyo Kamanda Nyombi aliwataja watuhumiwa wengine wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi ambao wanadaiwa kukimbia katika majibizano ya risasi na polisi kuwa ni Edson Mabisa(30)ambaye alikamatwa katika daraja lilipo katika jirani na Stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani ikiwa pamoja na Ally Mohamed (30) ambao wote ni wakazi wa mji mdogo wa Tunduma.

No comments:

Post a Comment