Ni Juhudi za Mkuu wa mkoa W.Lukuvi
OFISA Ardhi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Bw. Magesa Magesa amekamatwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. William Lukuvi kwa tuhuma za kugushi nyaraka mbalimbali na kuuza viwanja vya wazi katika eneo aghali ya Osterbay karibu na ufukwe wa Coco na Bwalo la maofisa wa Polisi jijini Dar es Salaam.
Nyaraka alizonasa Bw. Lukuvi zilikuwa na sahihi ya mkurugenzi wa manispaa hiyo inayodaiwa ya kughushi na muhuri wa ofisi hiyo.
Bw. Lukuvi alidai kupata taarifa kutoka kwa msiri wake, akavamia ofisi hizo ghafla na kukuta mafaili ya viwanja hivyo yakiwa mezani kwa Bw. Magesa yakijadiliwa na baadhi ya wafanyakazi.
Akizungmza na waandishi wa habari Bw. Lukuvi alisema kuwa wakati anatoka Ubungo Plaza katika ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) alipata taarifa kutoka kwa mtu mmoja ikimjulisha tukio hilo na ndipo alipovamia ghafla.
"Nilikuwa nimefika eneo la Jangwani, nilipopata taarifa nikageuza kwenda kuvamia ofisi hiyo. Nilikwenda nikinyemelea nyemelea, nilipopofika nikakuta kweli wanajadili mafaili hayo. Nikaomba wanishirikishe, na hapo ndipo kigugumizi kilianza," alisema Bw. Lukuvi.
Alisema kuwa nyaraka hizo zilionesha kwamba zimeandikwa mwaka 2009 na kuidhinisha ugawaji viwanja namba 1274 na 1275 kwa raia mmoja wa India mwenye Kampuni ya Tanzania Building Weihgt.
Alisema kuwa Bw. Magesa aliandika barua mbalimbali za uuzwaji wa viwanja hivyo na kuonekana zimepitishwa katika vitengo husika na kukubaliwa, kitu ambacho si kweli na viongozi waliotajwa wamekana kuhusika na nyaraka hizo.
Kwa mujibu wa Bw. Lukuvi, baada ya upekuzi zaidi walikuta nyaraka zingine ambazo zilionesha kuwa Mkuu wa Idara hiyo Bw. John Langasi naye amehusika kuweka saini na kuidhinisha baadhi yake.
Kasheshe ilizidi kuikumba ofisi yote baada ya watumishi wa idara hiyo kutakiwa kutoa nyaraka zingine na kuanza kusukumiana mpira, na wengine kutoweka ghafla katika ofisi hizo.
Kutokana na hali hiyo, Bw. Lukuvi aliagiza Bw. Magesa kukamatwa na kuwatoa nje watumishi 15 wa idara hiyo na kufunga ofisi hizo, na kuwaamuru kuondoka katika mazingira hayo ili kuepusha kuficha nyara hizo.
Watumishi walioondolewa ofisi hizo na kutakiwa kuripoti katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kila asubuhi ni makatibu muhtasi watatu, makarani wa masijala watatu, makarani wengine watatu na maafisa ardhi sita.
Bw. Lukuvi alisema kuwa leo watateua wafanyakazi wengine kutoka maeneo tofauti kufanya kazi katika ofisi za Kinondoni huku akisisitiza kwamba Bw. Langasi atahamishiwa nje ya Dar es Salaam.
Bw. Lukuvu alisema kuwa kwa mujibu wa mahojiano ya haraka haraka na Bw. Magesa amedai kuwa alishinikizwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa kutoa viwanja hivyo, na kwamba kuna vingine vingi vilivyouzwa kwa nguvu yao.
Bw. Lukuvi alisema kuwa amepata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wakidai kuwa kinara wa uuzwaji wa viwanja kiholela kiongozi mmoja wa kisiasa wa halmashauri hiyo.
Alisema kuwa kutokana hali hiyo amemwagiza Mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni kumkabidhi michoro yote ya viwanja vya manispaa hiyo, hasa vilivyokuwa wazi na kugawia kwa watu ili kuchunguzwa na kubaini kama vilitolewa kwa utaratibu maalumu.
Aliahidi kumkabidhi Mkurugenzi wa TAKUKURU Bw. Edward Hoseah majina ya watu wote, bila kujali wadhifa wao, walionunua viwanja vilivyokuwa wazi na kuwachunguza kama walifuata sheria na taratibu za kuvipata.
"Katika tathimini yangu niliyoifanya haraka haraka na kujumuisha na maelezo niliyopata wakati wa mahojiano, nimebaini viongozi wengi wa serikali waliopitia nyaja hiyo na wengine wanaohusika na ardhi watakuwa ndani ya migogoro huu kwa kuidhinisha nyaraka mbalimbali, hivyo lazime TAKUKURU iwafikie," alisema.
Bw. Lukuvi alisema kuwa amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuwapangia vituo vya watumishi watakaokuwa wanaripoti kwake huku upepelezi ukiendelea na ikibainika wameshiriki katika mchezo huo taratibu za kuwafukuza kazi zitafuatwa.
No comments:
Post a Comment