header

nmb

nmb

Wednesday, May 5, 2010

Askofu Mwakyolile asema mtandao wa mauaji ya watoto wadogo ni mkubwa


Askofu Mwakalolile akiendesha misa Tukuyu

KANISA la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde Mkoani Mbeya limesema kuna uwezekano wa kuwepo mtandao mkubwa wa mauaji ya kinyama ambao unatokana na imani za kishirikina na kuacha kumcha mwenyezi mungu.

Aidha imesema kuwa kila jambo mbele za mwenyezi mungu linawezekana,kikubwa amewataka watanzania kuungana na kufanya maombi ili kunusuru wimbi hilo la mauaji yaliouandama mkoa wa Mbeya.

Kauli hiyo imetolewa na Askofu wa kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde,Dkt. Ezlael Mwakyolile wakati alipokuwa kwenye Mahafari ya wahitimu wa Shahada ya ualimu na shahada ya Cheti katika Chuo cha ualimu cha Kirutheri kilichopo Uyole,jijini la Mbeya ambapo wanafunzi 24 walihitimu mafunzo hayo.


Askofu huyo amewaomba watanzania na waumini wa madhehebu ya dini kuuombea Mkoa kwani matukio ya mauaji yameuandama na kuujengea sifa na rekodi Mbaya ya mauaji na kutia aibu kwa viongozi wote wa chama na serikali sanjari na viongozi wa dini.

Mauaji ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano katika Wilaya ya Rungwe na Mbarali yameutikisa mkoa wa Mbeya hata kufikia Jeshi la polisi kuwashikilia watu 100 kutokana na mauaji ya Rungwe mpaka sasa wanaodaiwa kuhusika na matukio ya mauaji hayo ambayo yanadaiwa yalianza kufanyika Septemba mwaka jana na Aprili mwaka huu na idadi ya watoto sita kuuawa.
Aliwataka viongozi wa vijiji na wamiliki wa nyumba kuwa makini na wageni wanaoingia na kutoka kwani kuna dalili nyingi zinazoweza kuashiria kuwa kuna makundi yenye mtandao mkubwa katika maeneo jijini hapa.

"Ni vyema Kutoa taarifa kwa uongozi wa vijiji hususan kwa jeshi la polisi ili kuweza kubaini watu wanaojihusisha na matukio ya uhalifu na wamiliki wa nyumba wanaohifadhi watu wanaojihusisha na matukio ya uhalifu au kuhifadhi,"alisema.
Alisema kwa sasa mkoa umefikia pabaya ambapo panahitaji nguvu za ziada kwa kuongeza maombi ikiwa ni pamoja na jitihada za viongozi wa serikali kuongeza nguvu na kuhimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika kuimarisha mpango wa polisi jamii ulinzi shirikishi ikiwa ni pamoja na ulinzi wa jadi sungusungu.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,John Mwakipesile ameagiza kusitishwa kwa masomo ya jioni kwa watoto Wilayani Rungwe ili kunusuru mauaji ya wanafunzi na watoto wasiokuwa na hatia.

Asante mdau Thompson Mpanji, Mbeya.

No comments:

Post a Comment