header

nmb

nmb

Friday, April 23, 2010

WANANDOA WAUWAWA KWA TUHUMA ZA UCHAWI IR!!.HABARI ZA MAKAZI BORA NENDA CHINI!!

WATU wawili mke na mume wakazi wa kijiji cha Mawengi Wilaya ya Ludewa mkoani Iringa wameuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiofahamika kwa kuhusishwa na mambo ya ushirikina.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Bw. Evarist Mangalla alisema, watu wasiofahamika walivamia nyumbani kwa wanandoa hao na kufanya mauaji sambamba na kunyoa ndevu za mwanaume huyo kisha kutokomea nazo kusikojulikana.

Bw. Mangalla aliwataja waliouawa kuwa ni Bw. George Haule (75) na mkewe Bi. Agnes Kenjewala (55) wote wakazi wa kijijini hapo Mawengi na kwamba wanandoa hao walikuwa wakituhumiwa na watu mbalimbali kuwa walikuwa wakijihusisha na tabia za kishirikina.

Alisema tukio hilo lilitokea Machi 9 saa 5 usiku wakati wanandoa hao wakiwa nyumbani kwao na kwamba mjukuu wao aliyekuwepo wakati wa tukio hilo hajulikani aliko na kwamba inawezekana kuna jambo baya lilimpata baada ya kushudia mauaji hayo.

Hivi karibuni yalitokea mauaji mengine ya kikatili dhidi ya mtoto aliyefahamika kwa jina la Andrew Nchimbi (10) mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi Mahumbi, Ludewa mkoani hapa.

Katika tukio lingine mvua kubwa iliyonyesha siku tatu mfululizo katika Kata ya Manda wilayani Ludewa mkoani Iringa, imesababisha mafuriko katika vijiji vya Kipingu na Ngelenge huku mashamba ya mpunga, mihogo na mahindi yakizosombwa na kuharibiwa na maji.

Mbunge wa Jimbo la Ludewa Profesa Raphael Mwalyosi, alisema mvua hiyo ilianza kunyesha Machi 7 hadi 9 na kusababisha kitongoji cha kimoja cha Fockland kilichopo kata ya mto Luhuhu kuzingirwa na maji na kusababisha wananchi kukosa mawasiliano.

Bw. Mwalyosi alisema vitongoji vingine ambavyo vimeathiriwa na mafuriko hayo ni pamoja na Kipingu na Ngelenge ambako mashamba ya mpunga, mahindi, mihogo vimesombwa
Upande wake Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Ngelenge, Bw. Alanus Mbunda alisema kufuatia mafuriko hayo kumezuka wimbi la vijana wasio waaminifu wanaofanya uporaji wa mali za wananchi na kuiba mazao.

Bw. Mbunda alisema vijana hao wasiokuwa na utu wamekuwa wakitumia mitumbwi kusafirishia mazao hayo na kwamba wanahisiwa kutoka wilaya jirani ya Mbinga.

Amesema mafuriko hayo yameathiri zaidi mazao mashambani na kwamba hakuna taarifa za maafa kwa binadamu. Hasara kamili iliyosababishwa na mafuriko hayo haijafahamika .

No comments:

Post a Comment