header
nmb
Friday, April 16, 2010
CCM WADAI IMEJIPANGA VIZURI KWA USHINDI
Hivi karibuni Chama chetu (CCM) kilikamilisha kujipanga kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao, hali ambayo inatuhakikishia kuendelea kufanya vizuri katika uchaguzi ujao hasa ikizingatiwa vyama vya upinzani vimeshindwa kabisa kujipanga kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kutokana na kutokuwa na uongozi makini na imara ikiwa ni pamoja na wananchi kukosa kuwa na imani navyo. Kutokana na migogoro isiyokwisha na matatumizi mabaya ya mamilioni ya ruzuku wanayopata kutoka Serikalini.
CCM imejiandaa vizuri kwa kuendelea kujiweka karibu na uma wa Watanzania jambo ambalo limejidhihirisha hata katika matokeo ya Serikali za mitaa ambapo hakuna hata Chama kimoja cha upinzani kilichoweza kupata walau asilimia 2 huku CCM tukishinda kwa kishindo cha asilimia 93.
Katika kipindi hiki cha kuelekea katika Uchaguzi Mkuu tayari tumeshanunua magari aina ya Land Cruiser hard top 150 ambazo zimesambazwa katika wilaya zote nchini kurahisisha usafiri kwa viongozi wetu, hivi karibuni tunategemea kununua magari ya kutosha kwa ajili ya misafara ya wagombea wa Urais, Mgombea Mwenza wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar, pamoja na magari mengine 26 kwa ajili ya mikoa yote.
Utaratibu wa uchangiaji fedha kwa ajili ya uchaguzi huo uliozinduliwa hivi karibuni na Mwenyekiti wetu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete umepokelewa vizuri na wananchi hivyo kutarajia kufikia malengo yaliyowekwa.
Kamati za kufanikisha ushindi zimeshaundwa katika kikao kilichopita cha NEC kilichofanyika Mjini Dar es Salaam tarehe 8/4/2010 kama ifuatavyo:-
Kamati ya Utekelezaji ambayo ndiyo itakuwa na jukumu la kusimamia shughuli zote za kuleta ushindi Kamati hii itakayoongozwa na Katibu Mkuu Mhe. Yusuf Rajab Makamba (MB.(MNEC) na itajumuisha Wenyeviti wa Kamati nyingine zote zilizoundwa kwa ajili ya kuleta ushindi kama zifuatazo:-
Kamati ya Mkakati na Uenezi itakayokuywa chini ya Mhe. Abdurahman Omar Kinana, Kamati ya Fedha, Nyenzo na Vifaa vya Kampeni itakayokuwa chini ya Mhe. Zakhia Hamdan Meghji.
Ni mategemeo yetu kupata ushindi mkubwa zaidi wa kishindo kuliko ule wa mwaka 2005 ambao tulipata asilimia 80.3 kwa Urais wa Jamhuri ya Muungano, asilimia 53 kwa Urais wa Zanzibar na viti 206 vya Ubunge kati ya viti 232 vilivyopo sasa ambapo kati ya viti 182 vya upande wa Tanzania Bara CCM ina viti 176 na upinzani viti 6, kwa upande wa Zanzibar CCM viti 31 na CUF viti 19 bila ya kujumuisha viti maalum.
Ni mategemeo yetu kurejesha viti 6 vilivyo chini ya upinzani bara na kushinda viti vingi zaidi Zanzibar baada ya utekelezaji mzuri wa Ilani uliofanywa na Serikali zetu mbili.
Ni matarajio yetu vyombo vya habari vitaendelea kutoa fursa sawa kwa vyama vyote na kutojishirikisha katika utoaji wa taarifa zisizo na ukweli ambazo zinaweza kuleta machafuko katika nchi bila sababu yo yote ya maana.
Wenyewe mmeshuhudia jinsi Serikali zetu zilivyoweza kutekeleza ahadi zetu za 2005-2010, mmeshuhudia jinsi tulivyojipanga tayari kwa ushindi wakati wapinzani wetu wakiwa kimya na mikakati sifuri jambo linalotuhakikishia ushindi kwa lazima mwaka huu kama kauli mbiu yetu ya mwaka 2010 USHINDI NI LAZIMA.
Imetolewa na:-
Richard Hiza Tambwe,
NAIBU MKUU WA KITENGO CHA PROPAGANDA
15/4/2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment