MAJENEZA YENYE MIILI YA WACHUNGAJINI WALE WALIOFIA AJARINI NA KUTAKIWA KUFUFUKA
,Kenya
BAADA ya jitihada za maombezi ya kuwafufua wachungaji wawili wa Kanisa la Kingdom Seekers Fellowship la nchini Kenya kushindikana hatimaye waumini wa Kanisa hilo wameamua kuwazika viongozi hao.
Wachungaji hao walizikwa jana katika kaburi la pamoja huku waumini wa dhehebu hilo wakiwa bado na matumaini kuwa huenda wakafufuka.
Kabla ya mazishi hayo waumini hao waliungana na viongozi wa eneo hilo na maaskofu kusali sala ya kujaribu kuwafufua wachungaji hao, Patrick Wanjohi Wanja wa Jimbo la Nakuru na Francis Kamau Ndekei wa Jimbo la Nyahururu ambao walifariki katika ajali ya gari katika barabara kuu itokayo Nakuru kwenda Nairobi wiki iliyopita lakini sala zao hizo hizo zikagonga tena mwamba.
“Katika muda wa masaa mawili yajayo endapo hawatafufuka tutawazika ,”Askofu Harrison Ng’ang’a, aliwaambia waombolezaji waliokuwa nje ya Kanisa la Nakuru ambako ibada hiyo ilifanyika.
Hata hivyo baada ya ibada hiyo iliyochukua muda wa saa tano waombolezaji walielekea moja kwa moja katika makaburi yaliyopo eneo Nakuru Kaskazini ambako wachungaji hao wawili walizikwa katika kaburi moja.
Wachungaji hao walitakiwa kuzikwa Jumamosi iliyopita lakini waumini walikuwa na matumaini ya kuwa baada ya maombezi ya siku tano wachungaji hao wangeondokana na umauti.
Imeripotiwa kuwa maelfu ya watu walihudhuria mazishi hayo wakiwemo watazamaji waliokuwa wakitaka kushuhudia kama miujiza ya ufufuko wa wachungaji hao itakuwa kweli.
No comments:
Post a Comment