Desemba 3, mwaka jana mahakama ya rufaa ilisikiliza utetezi wa sababu za rufaa zisizopungua 10 kutoka kwa wakili wa warufani, Bw. Mabere Marando, ambaye aliiomba mahakama hiyo kuifutilia mbali hukumu ya Mahakama Kuu na kuwaacha huru wateja wake.
Mbali na Babu Seya, warufani wengine ni Johnson Nguza (Papi Kocha), Nguza Mbangu na Francis Nguza ambao kwa pamoja wanatumikia adhabu hiyo mpaka sasa.
Tangu kusikilizwa kwa utetezi huo wa rufani mwaka jana ndugu, jamii ya wanamuziki, familia ya wanasheria wamekuwa na shahuku ya kutaka kujua kama mahakama ya rufani itabatilisha hukumu hiyo au la, jambo linaloifanya siku ya kesho kusubiriwa kwa hamu.
Ofisi ya Wakili Marando ililithibitishia Majira jana kuwa Mahakama ya Rufaa imewapelekea hati ya wito mahakamani kwa ajili ya kutoa hukumu hiyo kesho.
Katika rufaa hiyo wanamuziki hao wanapinga adhabu ya kifungo cha maisha iliyotolewa mwaka 2004 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuridhiwa na Mahakama Kuu, huku warufani wakiwakilishwa na Bw. Marando baada ya wakili wao wa awali, Bw. Herbert Nyange kujitoa.
Matumaini ya mwisho kwa Bw. Nguza na familia yake yanabaki kwa hukumu ya majaji Salum Massati, Mbarouk S. Mbarouk wanaoongozwa na Nathalia Kimaro.
Babu Seya na wanawe walihukumiwa kifungo hicho baada ya mahakama kuridhika na ushahidi wa kesi ya kudhalilisha watoto wa kike, na baadaye hukumu hiyo kubarikiwa na Jaji Thomas Mihayo wa Mahakama Kuu.
No comments:
Post a Comment