Na Mwandishi Wa GPL. Mgombea Ubunge jimbo la Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Ijumaa hii ataweka kando gwanda maalum ambalo ni sare ya chama chake, na kulipa kisogo jukwaa la siasa, na atashika kipaza sauti ‘MIC’ na kudondosha shoo kali ya Hip Hop kama ilivyokawaida yake. Sugu, anatarajia kutoa shoo kwa kushirikiana na mastaa wengine wa muziki wa kizazi kipya kwenye Ukumbi wa Mtenda Sunset uliopo Mbeya. Wasanii ambao wametajwa kupanda jukwaa moja na Sugu siku hiyo (Septemba 17) ni Suleiman Msindi ‘Afande Sele’, Ferouz Mrisho Rehani, Abbas Hamis Kinzasa ’20 Percent’, Danny Msimamo, Fred Maliki ‘Mkoloni’, Gerald Mwanjoka ‘G Solo’, Mapacha ‘Maujanja’ na Isanga Family’. Akifafanua kuhusu kupanda jukwaani na kuvua kombati ya CHADEMA, Sugu alisema atafanya hivyo kama sehemu ya harambee ya kukusanya fedha za kumaliza kazi ya kulitwaa Jimbo hilo. “Wala siyo utani kaka, Ijumaa navua gwanda, navaa jeans. Nitakuwa na saa nzima ya kutoa shoo ya muziki kwa watu watakaohudhuria onesho hilo. Nataka niwaoneshe watu wangu wa Mbeya kile ambacho huwa nafanya. “Kuna watu wanasikia tu lakini hawajawahi kuona shughuli yangu jukwaani. Nitawaonesha. Wanakuja wakali kama Ferouz, Afande Sele, 20 Percent, Mkoloni, Msimamo, G Solo, Mapacha, Isanga Familiy na wengineo,” alisema Sugu na kuongeza: “Ni shoo maalum ya kuchangia kampeni. Tumegawa kadi maalum ambapo kuna maeneo zinanunuliwa kama njugu. Kila kadi tunauza shilingi 10,000. Tunapiga hatua kubwa na naamini tutafika kwa sababu tunapata sapoti ya kutosha kutoka kwa watu wangu kama ambavyo unaona wanamuziki wanaacha kazi zao wanakuja kushirikiana na mimi kaka yao kukusanya michango ili kuniwezesha.” Kuhusu maendeleo ya kampeni zake, Sugu alisema kuwa tumaini la ushindi linaongezeka kila siku kiasi ambacho haoni wapi ambapo anaweza kukosea na kutoa nafasi kwa mpinzani wake kupenya. Alisema, juzi alifanya mkutano uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Mbeya kwenye Uwanja wa Mbembela uliopo Kata ya Nzovwe, Iyunga na kuvunja rekodi ya mahudhuria ya ule wa uzinduzi wake uliochukua nafasi Uwanja wa Ruanda Nzovwe, Kwamama John. Kuhusu afya ya mshirika wake, Mkoloni aliyelishwa sumu, Sugu alisema: “Kwanza namshukuru Mungu anaendelea vizuri, leo (juzi) alikwenda tena hospitali kuangalia macho. Anaendelea vizuri, pengine waliompa sumu walitaka kummaliza ila yote tunayaacha apone kwanza, muhimu ni kwamba Ijumaa tutakuwa naye hapa kufanya shoo.” HABARI KWA HISANI YA (GPL)
No comments:
Post a Comment