header
nmb
Wednesday, August 25, 2010
MAGONJWA YAITIKISA PAKISTAN
ISLAMABAD,Pakistan
WAZIRI Mkuu wa Pakistan amesema kuwa Serikali yake ina wasiwasi mkubwa wa kutokea magonjwa ya milipuko kutokana na mafuriko makubwa yaliyoikumba nchi nchi hiyo.
Yousuf Raza Gilani ameyasema hayo katika mkutano wa madaktari waandamizi,maofisa wa Wizara ya Afya, Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN) na wajumbe mbalimbali kutoka taasisi zisizo za kiserikali na akasema kuwa Pakistan imekumbwa na balaa kubwa katika historia ya nchi hiyo.
"Wakati ufukala kwa wanadamu ukizidi kuongezeka,tuna wasiwasi mkubwa kuhusu kuzuka magonjwa ya milipuko,"alisema.
"Kuna uwezekano wa kutokea magonjwa yanayosababishwa na maji kama vile kipindupindu, kuhara na kuhara damu, hasa kwa watoto ambao tayari ni dhaifu na wanyonge."aliongeza.
Hadi sasa nchi hiyo bado imezingirwa na maji ya mafuriko lakini kuna baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ambayo watu wameanza kujenga upya.
Katika mafuriko hayo, maji yaliyokuwa na kasi yalisomba kila kitu na hata barabara na madaraja na inasemekana itachukua muda mrefu kwa nchi hiyo kurejea katika hali yake ya kawaida.
Hali hiyo imewafanya watu kukata tamaa na kushikwa na hasira.
Kabla ya mkutano huo, mapema Waziri Mkuu huyo alitembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko na kuonesha uso wa huruma na kuahidi misaada lakini watu wengi walionesha kushikwa na hasira huku wakituma ujumbe kwa Serikali kuwa msaada huo ni mdogo na umekuja ukiwa umechelewa.
Mratibu wa taifa wa Afya Pakistan alisema hali ya afya katika ukanda wa mafuriko ilikuwa chini ya udhibiti lakini bado tishio la kulipuka kwa magonjwa bado halijapita.
"Matatizo ya afya kwa kawaida uongezeka katika maeneo yaliyoathirika kwa mafuriko baada ya wiki nne hadi sita na tunahitaji kuwa waangalifu na kuwa tayari kukabiliana na hali hiyo," alisema Dkt. Jahanzeb Orakza.
Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC, Jill McGivering ameripoti kutoka katika mkutano huo wa mjini Islamabad akisema kuwa inaonekana kuwa mkutano huo ni jaribio kwa serikali kuboresha ushirikiano wake kutokana na kuongezeka kwa lawama jinsi inavyolichukulia tatizo hilo.
Wakazi wa eneo la Muzaffargarh lililopo katika Jimbo la Punjab waliiambia BBC kuwa wanaangaika ili kurejea katika hali zao.
"Wote ambao walinusurika wanapata chakula kinachohitajika. Watu wote ambao wamepoteza nyumba zao hawapati chochote," alisema mtoto mwenye umri wa miaka 11, Mansur Rizman.
"Wanatakiwa kuwapatia msaada watu wote ambao nyumba zao zimeteketea,"aliongeza.
Katika eneo la Nowshera, lililopo Kaskazini Magharibi mwa mji wa Islamabad,watu wamehifadhiwa kambini lakini pia wanailalamikia Serikali kwa jinsi wanavyohudumiwa.
"Tunachokipata ni chakula kilichopikwa tu na hakuna kitu kingine.Hakuna kitu chochote maofisa wanachukua misaada ya mablanketi,chupa za maji,vitanda lakini wanaviweka stoo,"mkazi mmoja wa kambi hiyo, Sher Ghani (48) aliliambia Shirika la Habari la Uingereza Reuters.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment