header

nmb

nmb

Tuesday, June 8, 2010

SI KWAMBA NAWABANIA ILA JIWEKENI SAWA ,KWANZA.TENDWA!!


MSAJILI wa vyama vya siasa Bw. John Tendwa, amesema kamwe hawezi kuyumbishwa na Chama cha Jamii (CCJ) kutishia kumpeleka Mahakani badala yake anaendelea kukitendei haki kwa kukihakiki hadi atakapomaliza ratiba yake kama alivyoipanga.
Akizungumza na Majira jana, Bw. Tendwa alisema haoni sababu za kubatilisha ratiba yake ya kuhakiki CCJ kwa kuwa ndicho kilichoombwa na Uongozi hivyo kinachofanyika kwa sasa ni kukitendea haki kwa kutekeleza kile walichohitaji wao na si vinginevyo.
"Mimi siwezi kuyumbushwa na upuuzi huo wa CCJ, kwanza walilalamika katika vyombo vya habari kwa maneno makali na mimi nina ushaidi, nikawaita tukaanza kuwahakiki, sasa Im doing my work brother, walitaka kutendewa haki sasa nawatendea haki,that is the story,"alisisitiza Bw. Tendwa.
Alipoulizwa kuhusu barua ya Uongozi wa CCJ kumtaka asitishe kazi hiyo tangu June 3 na uhalali wa kuendelea nayo bila Viongizi kuwepo alisema hawezi kufanyia kazi barua hiyo kwa kuwa chama hicho haina mamlaka ya kusimamisha shughuli zake akishapanga.
"Mimi sikuwaambia wasiwe na viongozi huko Mikoani, nimesajili vyama vingapi na si vyote nilikuwa na viongozi wao wa Kitaifa, kama hawana viongozi huko wameshindwa, lakini Ofisi yangu haiwezi kuendeshwa na CCJ, What is CCJ, eti wakitaka nikatishe uhakiki nifanye hivyo hapana,"alisisitiza Bw. Tendwa.
Alipoulizwa matarajio ya kazi yake baada ya uhakiki alisema atakapomaliza awamu hiyo ya kwanza kesho mjini Ungunja atawaita Viongoiz hao ili wamweleze kama wanataka aendelee na duru ya pili au wameshindwa.
"Kesho (leo) ndio watu wanaondoka kwenda Unguja keshokutwa (kesho) ndio uhakiki, baada ya kumaliza nitawaita hao viongozi waniambie kama wanataka niendelee ya duru ya pili au basi, kama watasema basi watakuwa wameshindwa and it will be the end,"alisema Bw. Tendwa.
Kuhusu CCJ kumshitaki alisisitiza msimamo wake kwamba waendelee na kesi ila yeye naye anaendelea na kazi yake ya uhakiki hadi hapo atakapomaliza ratiba yaje huku akiwatuhumu viongozi wa Chama hicho kutumia lugha isiyofaa kwake wakati walipomlalamikia.
Wakati Tendwa akitamba kuwatendea haki CCJ, Katibu Mkuu wa chama hicho Bw.Richard Kiyabo, alisisitiza kwamba uhakiki unaofanywa kwa sasa ni batili na inatokana kutumiwa kuhujuma chama hicho kwa madai kwamba ni tishio kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi Mkuu wa Octoba mwaka huu.
"Mwanasheria wetu anamalizia baadhi ya vipendele vya sheria, akimaliza tu tunakwenda kufungua Stop Order Mahakama Kuu leo (jana) licha ya kusitisha pili tunataka kufutwa kwa uhakiki aliyokwishafanya tangu Juni 3.
"Kazi yake ya kuendelea kuhakiki ni matokeo ya Tendwa kutumiwa kutuhumu, lakini apende asipende ni lazima atupatie usajili wa kudumu, ni haki yetu na tutaidai kwa kila mbinu,kama angetaka kuzingatia sheria baada ya barua yetu angetuita atusikilize kwanza akiona hatuna hoja ndio angeendelea ila hii ya kufanya anachotaka ni kutuhujumu,"alisisitiza Bw Kiyabo.
Alipoulizwa kuhusu uvumi kwamba Chama hicho kinafanya mpango wa kuunganisha nguvu na kile cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika uchaguzi Mkuu ujao alikanusha taarifa hizo na kuweka wazi kwamba iwapo kuna kiongozi alitoa kauli hiyo basi ni zake binafsi na si cha chama.

No comments:

Post a Comment