Kundi la wanamgambo Somalia lajiunga na SerikaliMOGADISHU,Somalia
KUNDI lenye nguvu la wanamgambo nchini Somalia la Sufi Muslim limejiunga na Serikali ili kukabiliana na kundi linalohusishwa na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, al-Shabab ambalo linashikilia maeneo makubwa ya nchi hiyo.
Makubaliano hayo ambayo yalisainiwa jana Makao Makuu ya Umoja wa Afrika AU yaliyopo nchini Ethiopia yanaonekana kuwa msaada muhimu kwa jeshi la Serikali lilanoungwa mkono na Umoja wa Mataifa (UN).
Kundi hilo ambalo pia ufahamika kama Ahlu Sunna Wal Jamaa ndilo linaloshikilia maeneo kadhaa katikati mwa Somalia ambapo pia limekuwa likiendesha mapigano na al-Shabab.
Makubaliano hayo yamepokewa kwa mikono miwili na Mkuu wa Kamisheni ya amani ya AU, Jean Ping akiyaita kuwa ni makubaliano ya kihistoria na akawataka wapiganaji wa al-Shabab na washirika wake kuweka silaha zao chini.
Hadi sasa Al-Shabab na washirika wake ndiyo wanashikilia eneo kubwa Kusini mwa nchi hiyo huku Serikali ya mpito inayoungwa mkono na waangalizi wa amani wa AU ikishikilia maeneo machache katika mji mkuu wa nchi hiyo,Mogadishu.
"Tumekubaliana kugawana madaraka,"alisema Waziri Mkuu wa Somalia, Omar Abdirashid Ali Sharmarke wakati wa hafla ya kusaini makubaliano.
Imeelezwa kuwa katika makubaliano hayo kundi hilo la Ahlu Sunna limepewa mawaziri watano na vikosi vyake kutoa ushirikiano kwa serikali katika mapambano ya kusaka amani.
No comments:
Post a Comment