header

nmb

nmb

Thursday, March 18, 2010

IPP NYANYA MBOVU KWA BTL YALAMBWA 6.0

Anaandika Victor Mkumbo,

TIMU ya soka ya Kampuni ya Business Times 'The Bize', jana imetinga katika fainali za michuano ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii 'NSSF Media Cup', baada ya kuiangushia gharika la mabao 6-0, timu ya IPP katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa TCC Sigara, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo mkali uliokuwa na ipinzani mkubwa, ulianza kwa The Bize kulishambulia lango la wapinzani wao IPP, ambapo katika dakika ya 10 ya mchezo huo mshambuliajia wake Julius Kihampa aliweza kuipatia timu hiyo bao la kwanza baada ya kuwatoka mabeki wa IPP na kuachia shuti lililojaa wavuni.

Katika dakika ya 41, mchezaji wa The Bize, Papapa Paulo aliiandikia timu yake bao la pili kwa kichwa baada ya kuonganisha krosi iliyotoka kwa Kihampa na kujaa wavuni.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu hizo kufanya mabadiliko kwa baadhi ya wachezaji ambapo mchezo ulianza kwa ulianza kwa The Bize kulishambulia lango la wapinzani wao IPP, ambapo katika dakika ya 53 walipata bao la tatu mfungaji akiwa Sunday George baada ya kuachia shuti kali lililomshinda kudaka, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Rehule Nyaulawa.

Wakitandaza kandanda safi, The Bize walipata bao la nne lililowekwa kimiani na mfungaji wake Papapa baada ya kuonganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na Mohamed Akida na kujaa wavuni.
Mwamuzi wa mchezo huo, Japhari Mchira alimzawadia kadi nyekundu mchezaji wa IPP, Seif Majala, baada ya kumchezea rafu Sunday George katika dakika ya 76.

Mchezaji wa The Bize, Papapa ambaye alionekana kuwa mwiba mkali kwa upande wa IPP, aliipatia timu yake bao la tano katika dakika ya 77, baada ya kuonganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa na Geore Dennis na kujaa wavuni moja kwa moja.

The Bize walijihakikishia kucheza fainali za michuano hiyo, baada ya kutumbukiza nyavuni bao la sita katika dakika ya 87 kupitia kwa Dismas Bahati baada ya kuachia shuti kali lililomshinda kudaka mlinda mlango wa IPP, Said Kandamba na kujaa wavuni.

No comments:

Post a Comment