KUNDI la viongozi mashuhuri wa Muungano wa Afrika limeelezea wasiwasi wake kuhusu mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini Kenya, na kusema kuwa huenda ukaathiri utekelezwaji wa mkataba wa kitaifa wa serikali ya muungano.
Katika taarifa yao, kundi hilo linaloongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) na mpatanishi mkuu katika mzozo nchini Kenya, Kofi Annan, limewataka rais Mwai Kibaki na waziri Mkuu Raila Odinga wafanye mashauriano ili kuutatua mzozo huo.
Mvutano wa hivi karibuni kati ya Rais Kibaki na Waziri Mkuu Odinga ulianza Jumapili iliyopita baada ya Rais Kibaki kubatilisha uamuzi wa awali wa Odinga kuwasimamisha kazi mawaziri wawili waliohusishwa na kashfa za ufisadi.
Kutokana na hatua hiyo, Odinga alitoa wito kwa Annan kuja kuutatua mzozo huo.
Lakini taarifa ya jopo hilo la watu mashuhuri imemnukuu Annan akitoa wito kwa waakilishi wa pande mbili walioshiriki katika kubuni mwafaka wa serikali ya muungano kutilia mkazo kutekeleza agenda za mwafaka huo.
Jopo hilo limeelezea wasi wasi kwamba huenda mzozo uliopo ukatatiza juhudi za kupambana na ufisadi katika serikali ya Kenya.
Awali Rais Kibaki alisema hakuna mzozo wowote katika serikali ya Kenya huku jana Waziri Mkuu Odinga akikaririwa akiwa ziarani nchini Japan akisema kuwa mzozo huo hautavunja Serikali hiyo ya muungano.
No comments:
Post a Comment