Mkurugenzi wa Lino International Agency Limited, Bw. Hashim
Lundenga (kulia) akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
kuhusu safari ya Mrembo wa Tanzania wa mwaka 2013 kuelekea katika Mashindano ya
Urembo wa Dunia (Miss World 2014) nchini Uingereza.
Na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM.
MREMBO wa Tanzania wa mwaka 2013, Happiness Watimanywa ameahidi
kuing’arisha Tanzania katika mashindano ya ulimbwende ya Dunia yatakayofanyika
mapema mwezi ujao huko nchini Uingereza.
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,
mlimbwende huyo amewaeleza waadishi kuwa, kutokana na uzoefu wa kazi zake
alizokuwa akifanya kwa jamii kwa muda kipindi cha mwaka mmoja ikiwemo misaada
ya hali na mali anayoipata toka Bodi ya Utalii Tanzania pamoja na
wahisani wengine nchini amewaahidi Watanzania kuibuka na ushindi katika
kinyang’anyiro hicho huko nchini Uingereza ili kuitangaza Tanzania.
Alieleza kuwa, tayari Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza
utakuwa tayari kumpokea pindi atakapowasili nchini humo kwa lengo la
kuiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo ya ulimbwende yatakayowahusisha
walimbwende toka Ulimwengu mzima.
“Nimejifunza mambo mengi hasa kipindi wakati nasafiri sehemu
mbalimbali nchini pamoja na kufanya kazi za kusaidia jamii katika kipindi
chote, hivyo nawaahidi watanzania ushindi katika mashindano hayo
yatakayofanyika huko Uingereza pia mnipigie kura zenu za wingi”, alisema
Watimanywa.
Naye Mkurugenzi wa Lino International Agency Limited, Bw. Hashim
Lundenga ambao ni waandaaji wa Miss Tanzania, alisema kuwa mashindano ya Urembo
wa Dunia ni mashindano ya Kimataifa ambayo yanawakutanisha walimbwende toka
nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania, hivyo alitoa wito kwa watanzania wote
kuunga mkono kwa kumpigia kura nyingi mwakilishi ambaye ndiye mrembo wa
Tanzania kwa mwaka 2013, Hapinness Watimanywa ili ajinyakulie taji hilo la
dunia ili aweze kuipa sifa Tanzania kimataifa.
No comments:
Post a Comment