header

nmb

nmb

Monday, October 13, 2014

MPULIZA SAXAPHONE WA ZAMANI WA MSONDO NGOMA, ALLY RASHID AFARIKI DUNIA, AZIKWA



HAWA ni baadhi ya wanamuziki wakongwe waliohudhuria mazishi ya Ally Rashid

 Ally Rashid, wa tatu kulia akiwa na wanamuziki wenzake wakongwe
Jeneza lenye mwili wa marehemu Ally Rashid likipelekwa makaburini

Mwanamuziki wa zamani aliyekuwa mpiga saxaphone aliyejulikana pia kama Mzee Saboso, Ally Rashid amefariki dunia jana mchana.  Mzee Ally kwa mara ya mwisho alikuwa bendi ya Msondo Ngoma.

Umati mkubwa wa watu ulijitokeza kumzika Ally Rashid mwanamuziki wa siku nyingi ambaye alifariki jana mchana. Mazishi yalifanyika katika makaburi ya Keko Machungwa, kaburi lake likiwa jirani kabisa na la mwanamuziki mwingine nguli Moshi William.

Mazishi ya Mzee Alyy yalifanyika muda wa saa nne asubuhi na pia kuhudhuriwa na wanamuziki wengi wa zamani na hata wa sasa, akiwemo Mchizi Mox, ambaye alikuwa kimwita marehemu baba yake mdogo

HISTORIA YA ALLY RASHID KHAMIS ‘SABOSO’

Ally Rashid ‘Saboso’, huyo ni mpulizaji nguli wa ‘Saxophone’ aliyewahi kuzitumikia bendi kadhaa za hapa nchini na kutokea kujizolea sifa kemkemu kutokana na umahiri wake wa kucheza na chombo hicho.

Hivi tunavyozungumza Saboso amepoteza uwezo wa kupuliza Saxophone kutokana na kuwa, anasumbuliwa na maradhi ya kupooza kwa muda mrefu sasa.Mwandishi wa makala hii alimtembelea Saboso nyumbani kwake Keko, jijini Dar es Salaam anapougulia na kuongea naye mengi kuhusiana na maisha yake, muziki pamoja na maradhi yanayomsumbua.

“Maradhi haya yamenianza miaka kadhaa nyuma, nikiwa na bendi yangu ya Msondo Ngoma, siku moja tulikuwa natumbuiza kwenye ukumbi mmoja kule Mbagala Rangi Tatu, ambao jina lake silikumbuki vema,” anasema Saboso.

“Wakiwa katikati ya shoo, ghafla aliibuka mwanamke mnene aliyevaa nguo nyekundu na kumuomba kucheze naye, lakini alimkatalia kutokana na desturi yake ya kutokupaparika na wanawake, hususan akiwa kazini. Yule mwanamke alimlazimisha sana kucheza naye na alivyoonekana kuwa kero, Mabera aliamrisha atolewe kinguvu, lakini kabla hilo halijafanyika, aliyeyuka na hapohapo Saboso akaanza kuishiwa nguvu. Saboso anasema kuwa, alianza kuhisi ulimi wake unakuwa mzito na kutokea kwa dalili nyingine za kupooza ambapo aliamua kukaa chini baada ya kushindwa kusimama.

“Dansi lilipomalizika Romario alinisindikiza nyumbani kwa vile njia yetu ni moja tukaachana mbele, lakini nilipomgongea mlango mke wangu na kunifungulia, alionekana kunishangaa sana,” anasema Saboso.

Saboso alipoingia ndani aliamua kumuuliza mke wake juu ya mshangao wake, akamwambia kuwa wakati ananifungulia mlango, alimuona mwanamke kasimama nyuma yake na baadaye akayeyuka na kupotea.

Baada ya matukio hayo, hali ya maradhi iliendelea kumsumbua Saboso na takriban miezi miwili baadae alipata nafuu na kurejea kazini baada ya familia yake kumuhangaikia mno.

“Lakini miezi sita hivi baada ya kupona, siku moja nikiwa kwenye baiskeli yangu maeneo ya Kamata, Kariakoo naelekea kazini, nikaanguka ghafla na kupoteza tena nguvu,” anasema Saboso. Alichomudu kukifanya pale ni kuita taksi ya karibu iliyompeleka ofisini kwao Ilala, ambapo wanamuziki wenzie walipomuona waliamua kumuwahisha Hospitali ya Amana.

Saboso anasema kuwa, akiwa Amana ndipo alikatikiwa kabisa na kauli akawa hajimudu kuzungumza. Familia yake ikaanza tena kumuhangaikia hadi leo bila dalili yoyote ya mafanikio.

Saboso anasikitika akisema, bendi yake ya Msondo Ngoma imemsusa na kumtelekeza kabisa, licha ya kuwa alipatwa na matatizo hayo wakati akiwa kazini.

Anasema, ana miaka minane sasa kitandani na katika miaka yote hiyo, hajapata msaada kutoka Msondo, zaidi ya kutembelewa mara chache huko nyuma na baadhi ya wanamuziki wa bendi hiyo ambao si viongozi.

“Nawakumbuka waliowahi kunitembelea, wengine ikiwa ni mara moja tu, ambao ni Romario, Hamis Mnyupe, Ibrahim Kandaya, Huluka Uvuruge na Ismail Mapanga ambaye kwa sasa ni marehemu,” anasema saboso.

Anasema kuwa, Meneja wao, Said Kibiriti alifika mara moja tu kumjulia hali na kukata mguu akiwa kasahau kwamba, naye alishiriki majadiliano ya kukopa vyombo Unguja, baada ya Jumuia ya Wafanyakazi kujitoa.

Historia ya Saboso kimuziki inaanzia mwaka 1952 alipokuwa mpiga ngoma wa bendi ya Zanzibar Jazz, baadae akahamia Afrika Jazz ya hukohuko Zanzibar alipoanza pia kuimba.

Mwaka 1959 alihamishia virago jijini Dar es Salaam alipojiunga na bendi ya Dar es Salaam Jazz iliyomkutanisha na wanamuziki Nassor Mtondoo, Grey na Uporoto, akabahatika kurekodi hapo kibao ‘Shukrani Natoa’.

“Mwaka 1960 nikatua Western Jazz, Wema Abdallah akanipokea na hapo nikakubalika zaidi kwa mashabiki kiasi cha kupachikwa jina hili, ‘Saboso’ kutokana hasa na kushiriki kuimba wimbo ‘Saboso’,” anasema.

Saboso anasema kuwa, akiwa Western Jazz, Saboso aliimba pia vibao kama ‘Jela ya Mapenzi’, ‘Ulokusudia Mwenzangu’ na ‘Veronica’ huku vilevile akishiriki kupuliza Saxophone ndogo aliyojifunza kidogokidogo wakati ule alipokuwa kisiwani Unguja.

Mwaka 1972 akachomoka Western Jazz na kujiunga na bendi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Kimbunga Stereo), alipokutana na magwiji wengi akiwamo Kapteni John Simon.

Akiwa hapa, ‘Baba Mwenye Nyumba’ ni kati ya vibao ambavyo Saboso alipuliza Saxophone kwa ufundi mkubwa, kabla ya mwaka 1977 kutimkia Orchestra Double O ya Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kii’ ambako hata hivyo hakuwahi kurekodi.

“Mwaka 1978 niliingia Orchestra Bima Lee iliyokuwa ikitumia mtindo wa ‘Magnet Tingisha’ na kukutana na wababe wa muziki kama Joseph Mulenga, Shaaban Dede, Jerry Nashon, Othman Momba na Hamis Sama,” anasema Saboso.

Saboso ambaye ni kati ya waasisi wa bendi ya Shikamoo Jazz, aliorekodi na kusafiri nao sehemu mbalimbali duniani, anajivunia kupuliza Saxophone ya kiutu uzima kwenye vibao vingi vya Bima Lee vikiwamo‘Pesa’, ‘Visa vya Mesenja’ na ‘Baba Mwamvua’.

Balaa la Saboso halikukomea huko tu, bali hadi katika miaka ya hivi karibuni alipoingia Msondo Ngoma na kushiriki kikamilifu kwenye albamu mbili ambazo ni ‘Kaza Moyo’ na ‘Ajali’.

Unapomuuliza kuhusu kazi alizozifanya mwenyewe ambazo zinamvutia hata anapozisikiliza hivi sasa, Saboso anayejivunia umaarufu katika muziki, anakutajia vibao ‘Baba Mwamvua’ na ‘Pesa’ vya Bima Lee.

Nyumba anayoishi Saboso aliyewafundisha kupuliza Twahili Mussa na Mafumu Bilali ‘Bombenga’ kupuliza Saxophone, aliijenga mwaka 1961 alipoajiriwa kiwanda cha nguo kilichokuwa kinajulikana kama Tanganyika Textile Mills.

“Hapo nilikuwa mpishi wa rangi za mashuka na mwanamuziki pia, ambapo nilikopeshwa sh. 300, sh. 100 nilinunua kiwanja na kuanza kujenga taratibu, huku mabati nikikopeshwa na Bima,” anasema Saboso.

Alizaliwa miaka 75 nyuma, Ndagoni Pemba na elimu yake ya msingi aliichukulia jijini Tanga katika miaka ambayo haikumbuki kabisa hivi sasa. Mzee Ally Rashid amefariki leo 10 Oktoba 2014.
MUNGU AMLAZE PEMA PEPONI   HABARI NA MAKALA HII IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA WANAMUZIKI WETU YA JOHN KITIME.

No comments:

Post a Comment