Dodoma. Bunge limeanza mchakato wa kutunga Kanuni za
Maadili na Mwenendo wa Wabunge ambazo zinalenga kuwabana, ikiwamo hatua
ya kuwapiga marufuku kuwa na nyaraka za siri zinazohusu utendaji wa
Serikali bila kibali cha mamlaka zinazohusika na utunzaji wa siri hizo.
Habari ambazo zilipatikana juzi bungeni Dodoma zinasema kanuni za
maadili kwa wabunge ni matokeo ya kuwapo kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo
za rushwa, ambazo zimekuwa zikielekezwa kwao, lakini Bunge limekuwa
likishindwa kuchukua hatua kutokana na kutokuwapo kwa kanuni husika.
Hata hivyo, tayari baadhi ya wabunge wameonyesha kuzipinga kanuni hizo
kwa maelezo kwamba zinalenga kuwanyima uhuru wa kutekeleza majukumu yao
kiufanisi.
Mmoja wa wabunge wa CCM anayetoka Mikoa ya Kanda ya Magharibi akiwa
ameshikilia rasimu hiyo mbele ya waandishi wa habari alisema: “Hawa
wanataka kutufanya kama watoto wa shule, sisi hatutakubaliana na hii
kitu, tukikubali tu tunageuzwa watumwa”.
Kanuni hizo ambazo ziko kwenye ngazi ya rasimu,utunzi wake unaratibiwa
na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge chini ya Mamlaka ya
Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge inayolipa mamlaka Bunge
kuandaa kanuni za maadili kwa wabunge.
Kanuni za maadili zinazopendekezwa pia zinatilia nguvu msingi wa utunzaji siri za Ofisi ya Bunge na nyaraka zote za siri.
Rasimu ya kanuni hizo ambayo gazeti hili limeiona pia zinasema mbunge
hatatumia taarifa atakazozipata kwa wadhifa wake wakati akitekeleza
shughuli za Bunge au Kamati ya Bunge
No comments:
Post a Comment