Hatimaye vikosi vya usalama nchini Kenya vinasema
vimelidhibiti jengo zima la Westgate mjini Nairobi, ikiwa ni zaidi ya
siku tatu baada ya jengo hilo kuvamiwa na wanamgambo.
Milipuko ikifuatiwa na milio ya risasi imesikika
kutoka ndani ya jengo hilo asubuhi ya leo huku duru zikisema kuwa
vikosi vya usalama vinaelekea kukamilisha operesheni hiyo.
Serikali imesema zaidi ya watu 60
wameuawa na wengine zaidi ya 170 kujeruhiwa katika shambulio hilo
ambalo Al shabaab imekiri kulitekeleza.
Wizara ya mambo ya ndani imesema wanajeshi
wanaendelea kulisaka jengo zima la Westgate kutoka gorofa moja hadi
nyengine kuhakikisha kwamba hakuna mateka aliyesalia
Wakati huohuo, waziri wa mambo ya nje amesema
kuwa wawili kati ya wanamgambo watatu waliofanya shambulii hilo ni raia
wa Marekani pamoja na mwanamke muingereza.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni
nchini Marekani, Amina Mohamed alisema kuwa wamarekani walikuwa kati ya
umri wa miaka 18 na 19 ingawa wenye asili ya kisomali au kiarabu na
waliishi mjini Minnesota. Alisema kuwa mwanamke huyo muingereza alikuwa
amefanya vitendo vingi vya aina hii kwa niaba ya Al Shabaab.
Shirika la Red Cross limeambia BBC kuwa watu 63 wangali hawajulikani waliko.
Haijulikani idadi ya wanamgambo waliokuwa ndani
ya jengo hilo , lakini maafisa wa usalama wamesema kuwa wanamgambo
watatu wameuawa.
Kundi la kigaidi la al-Shabab limekiri
kutekeleza mauaji hayo, kulipiza kisasi hatua ya Kenya kujihusisha
kijeshi nchini Somalia.
Operesheni hiyo iliendelea usiku kucha ingawa kwa mujibu wa waziri wa usalama wa Kenya, ilikuwa katika mkondo wake wa mwisho.
"magaidi hawa huenda wanakimbia na kujificha
katika sehemu mbali mbali za jengo hilo lakini ghorofa zote za jengo
hilo zimedhibitiwa na majeshi,'' alisema Ole Lenku
Aliongeza kuwa mateka wote walifanikiwa kuokolewa.
Jumatatu jioni moshi mkubwa ulionekana ukifuka
kutoka kwenye jengo la Westgate ukiambatana na moto mkubwa. Moto huo
unasemekana uliwashwa na wanamgambo hao ili kutatiza vikosi vya usalama
katika juhudi zao za kutaka kukomboa jengo hilo.
sourc: www.bbc.co.uk/swahili
No comments:
Post a Comment