Wanawake wawili raia wa Tanzania
wametambuliwa kuwa ndiyo wanaodaiwa kuingiza shehena ya dawa za kulevya
zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 6.8 nchini Afrika Kusini wakitokea
Tanzania.
Akizungumza na NIPASHE jana,
Kamanda wa Polisi Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya,
Geofrey Nzoa, alisema haijafahamika wanawake hao wanatoka mikoa gani.
Kamanda Nzoa aliwataja wanawake hao kuwa ni Agnes Jerald ambaye alisema hajapiga hesabu ya umri wao, ila alizaliwa mwaka 1988 kwa maana hiyo ana umri wa miaka 25 na Melisa Edward ambaye
alisema amezaliwa mwaka 1989 kwa maana hiyo atakuwa na umri wa miaka
24. Wawili hao bado wanaendelea kuhojiwa na polisi wa Afrika Kusini.
Alisema Jeshi la Polisi Nchini
kwa upande wake linaendelea kufanya uchunguzi kubaini kama dawa hizo
walitoka nazo wapi na pia linawasaka watu ambao watakuwa ndiyo wamiliki
wa dawa hizo.
Jumapili iliyopita NIPASHE
ilipata taarifa za kukamatwa kwa dawa za kulevya aina ya Crystal
Methamphetamine zenye thamani hiyo nchini Afrika Kusini wakati
zikisafirishwa kutoka Tanzania.
Taarifa hizo zilionyesha kuwa
wanawake wawili walikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Oriver Tambo uliopo eneo la Kempton Park siku ya Ijumaa wiki iliyopita
wakitokea Tanzania.
Wanawake hao walikamatwa na
maofisa wa Mamlaka ya Mapato ya Afrika Kusini wakiwa na masanduku sita
ambayo yalipokaguliwa yalikutwa na takribani kilo 150 za dawa hizo
ambazo pia zinajulikana kama ‘Tik’ zikiwa na thamani ya bei ya mtaani ya
Randi milioni 42 sawa na Sh. bilioni 6.8.
Baada ya kukamatwa na dawa hizo wanawake hao walikabidhiwa polisi.
Tukio hilo linatoka takribani
wiki moja baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Juni 28, mwaka huu
kutangaza kuwa tatizo la dawa za kulenya hivi sasa ni janga la kitaifa
nchini.
Alisema kumekuwa na wimbi kubwa
la Watanzania wanaojiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya
ndani na nje ya nchi na kwamba, katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita, watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na dawa hizo.
Pia alisema katika kipindi hicho,
Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika
Kusini, na hivyo kuharibu taswira ya nchi na kusababisha Watanzania
wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu wanapotaka kusafiri
kwenda nchi mbalimbali duniani.
Pinda alisema mwaka huu pekee
kumekuwa na ukamataji mkubwa wa dawa za kulevya katika eneo la kimataifa
la Bahari ya Hindi karibu na Tanzania.
Alisema hivi sasa mikate, maandazi na askrimu zinazouzwa kwenye shule za msingi, zinawekwa dawa za kulevya.
Alisema vitendo hivyo vinafanya
vijana wengi wa shule za msingi na hata sekondari kuwa na tabia za
ajabu, ikiwamo kuingia darasani wakiwa na kiatu kimoja mguuni, mkufu
wenye nyembe na kidani chenye nyembe kifuani.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment