Makachero wa FBI kutoka Marekani wamewasili nchini
Tanzania kusaidia katika upelelezi wa shambulizi la bomu lililotekelezwa
katika kanisa katoliki mjini Arusha siku ya jumapili.
Mwandishi wa BBC Baruan Muhuza akiwa mjini
Arusha anasema makachero hao wa FBI wako Tanzania kusaidiana na Jeshi la
wananchi wa Tanzania na Polisi kutafuta undani wa tukio hili ambalo
limeishtua na kuiweka serikali ya Tanzania katika wakati mgumu.
Baruan Muhuza anaongezea hali inaonekana kuwa ngumu zaidi hasa
kutokana na aina ya matukio ambayo yamekuwa yakitokea katika siku za
hivi karibuni yakihusisha viongozi wa dini ambapo wengi ya wanaodhurika
huwa ni wa imani ya kikristo.
Wakati huo huo wakuu wa serikali wakishirikiana na viongozi wa kidini wameandaa mkutano utakaojumuisha viongozi wapatao 200.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadiq
amewaambia wanahabari kuwa wamelazimika kuandaa mkutano huo wa siku
mbili kufuatia agizo la Rais Jakaya Kikwete.
Mkutano huo utajadili uhusiano bora baina ya wakrito na waislamu.
Polisi nchini Tanzania inawashikilia watu wa nane kwa
madai ya kuhusika na mlipuko wa siku ya jumapili katika kanisa Katoliki
la Olasit viungani mwa mji wa Arusha.
Miongoni mwa washukiwa ambao wako mikononi mwa polisi ni raia wanne wa Saudi Arabia, na wengine wanne ni raia wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment