TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Machi 19, 2013
Kiingilio cha chini katika mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas) itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.
Viti vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kumeza watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045 ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio vya daraja la juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni sh. 15,000 wakati sh. 20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A yenye watazamaji 748 kiingilio chake ni sh. 30,000.
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza kuuzwa siku mbili ya mchezo (Ijumaa na Jumamosi) katika vituo vifuatavyo; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni na Dar Live Mbagala.
Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya mauzo ya tiketi uwanjani siku ya mechi. Vilevile tunapenda kuwakumbusha watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi hiyo.
SAMATA, ULIMWENGU WARIPOTI STARS
Washambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wamewasili nchini jana usiku na kwenda moja kwa moja kambini.
Ujio wa washambuliaji hao unafanya idadi ya wachezaji walioripoti kambini kufikia 20 kati ya 23 walioitwaa baada ya mshambuliaji Khamis Mcha aliyekuwa na kikosi cha timu yake ya Azam nchini Liberia naye kuripoti kambini leo asubuhi.
Wachezaji John Bocco na makipa Mwadini Ally na Aishi Manula ambao pia nao walikuwa Liberia na timu yao ya Azam wataripoti kambini leo alasiri. Wachezaji hao ni sehemu ya msafara wa timu ya Azam ambao utakuja na ndege ya mchana kutokea Nairobi kwa vile ile ya asubuhi waliyotangulia nayo wenzao kuwa imejaa.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha Kim Poulsen leo inaendelea na mazoezi Uwanja wa Taifa. Mazoezi hayo yataanza saa 9 alasiri.
TIMU TATU ZASHUKA DARAJA FDL
Timu tatu zimeshuka daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kurudi Ligi ya Mkoa msimu ujao wa 2013/2014 baada ya kushika nafasi za mwisho katika ligi hiyo msimu huu 2012/2013 iliyomalizika wikiendi iliyopita.
Small Kids ya Rukwa imeporomoka kutoka kundi A baada ya kuondolewa kwenye michuano hiyo mapema kwa kushindwa kufika uwanjani kwenye moja ya mechi zake. Kwa mujibu wa kanuni matokeo yote ya mechi ilizocheza yalifutwa.
Moro United ya Dar es Salaam ndiyo iliyoaga FDL kutoka kundi B baada ya kumaliza mechi zake ikiwa na pointi tatu. Wakati kutoka kundi C timu iliyoshuka ni Morani ya Manyara iliyomaliza ligi ikiwa na pointi kumi na moja.
Timu zilizopanda daraja kucheza Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2013/2014 ni Mbeya City ya Mbeya iliyoongoza kundi A ikiwa na pointi 31, vinara wa kundi B timu ya Ashanti United ya Dar es Salaam yenye pointi 29 wakati Rhino Rangers ya Tabora imepanda kutoka kundi C ikiwa na pointi 32.
LIUNDA KUTATHIMINI WAAMUZI KOMBE LA DUNIA
Mwamuzi Msaidizi wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Leslie Liunda ameteuliwa kuwa mtathimini wa waamuzi (referee assessor) kwenye moja ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia.
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limemteua Liunda kutathimini waamuzi kwenye mechi kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Libya itakayochezwa Jumapili (Machi 24 mwaka huu).
Mechi hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Martyrs jijini Kinshasa kuanzia saa 9.30 alasiri kwa saa za Afrika ya Kati (CAT).
Waamuzi watakaochezea mechi hiyo William Selorm Agbovi atakayekuwa mwamuzi wa kati, Malik Alidu Salifu (mwamuzi msaidizi namba moja), David Laryea (mwamuzi msaidizi namba mbili) na mwamuzi wa mezani (fourth official) Cecil Amatey Fleischer. Waamuzi wote hao wanatoka Ghana.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment