header

nmb

nmb

Tuesday, March 12, 2013

AMINA NGALUMA(JAPANIZI) APANIA KUANZISHA BENDI YAKE YA MUZIKI





MWANAMUZIKI machachari wa kike nchini, Amina Ngaluma amesema moja ya ndoto alizonazo ni kuanzisha na kumiliki bendi yake ya muziki wa dansi.

Amina, ambaye kwa sasa anaimbia bendi ya Jambo Surviver, inayopiga muziki nchini  Thailand, alisema iwapo mipango hiyo itafanikiwa, bendi hiyo itakuwa ikifanya maonyesho yake kwenye hoteli za kitalii.

Mwanadada huyo, ambaye amewahi kuimbia bendi mbalimbali nchini, zikiwemo African Revolution na Double M Sound, alisema hayo wiki hii kupitia barua pepe aliyotuma kwa mwandishi wa habari hii.

"Kwa sasa nipo Thailand, napiga muziki katika bendi ya Jambo Surviver, inayoundwa na baadhi ya watanzania. Nipo huku nikitafuta maisha,"alisema Amina, ambaye kabla ya kujitosa katika muziki wa dansi, aliwahi kuimba muziki wa taarab katika kikundi cha wazazi.

"Nitakaporudi Tanzania, kama Mungu atanijalia, lazima nianzishe bendi yangu. Nataka iwe bendi ya ukweli," aliongeza.

Kabla ya kwenda Thailand, Amina alifunga ndoa na mwanamuziki Rashid Sumuni, waliyekuwa pamoja katika bendi ya Double M Sound. Sumuni alikuwa mpiga solo wa bendi hiyo.

Amina alisema siyo kweli kwamba ameacha muziki, isipokuwa aliamua kuondoka Tanzania kwenda kupiga muziki Arabuni na baadaye kutimkia Thailand.

Alisema anamshukuru Mungu kwamba maisha yake yanakwenda vizuri hivi sasa kwa vile muziki wa kwenye hoteli unalipa ikilinganishwa na muziki wa kwenye maonyesho ya kumbi za burudani.

Kwa mujibu wa Amina, katika bendi hiyo, wanapiga muziki wa kuiga wa wasanii na bendi mbalimbali maarufu duniani kwa vile ndio unaopendwa zaidi.

Mbali na kupiga muziki wa kuiga, Amina alisema wakati mwingine huwa wanapiga nyimbo zao zenye vionjo na miondoko ya Kitanzania.

"Kuwepo kwangu huku hakuna maana kwamba maisha yangu yote yatakuwa Thailand. Nimekuja huku kutafuta,"alisisitiza.

Amina alisema kwa sasa anakusanya nyimbo zake zote alizowahi kutunga na kuimba katika bendi mbalimbali kwa ajili ya kutengeneza albamu.

No comments:

Post a Comment