header

nmb

nmb

Thursday, November 1, 2012

Hatari lakini Salama!!

 

Pamoja na ujenzi mzuri wa kituo hiki cha abiria wavukao kutoka Sengereama kwenda Mwanza mjini kwenye Ziwa Victoria, lakini suala la usalama hapa ni ziro kabisa, magari hayo pichani yakisubiria kivuko lakini hakuna kizuizi chochote kinachozuia hata kwa dharura kama ikitokea bahati mbaya gari moja kugonga mwenzake. Lakini hata hivyo hakuna sababu yoyote ya magari haya kusubiri kivuko kwenye eneo hili la karibu na maji wakati eneo la kutosha lipo.
Magari yakiwa kwenye foleni ya kuingia kwenye Kivuko cha Mv Misungwi, umbali wa kuvuka kwenye eneo hili nitofauti na ule umbali wa Kigamboni na Posta ambao huchukua dakika tano , hapa ni mwendo wa dakika 20 kufika ng'ambo ya pili.
Tatizo la kuondoa Kivuko kabla ya watu hawajaishi kuingia nalo hujitokeza maeneo mengi ya vivuko sababu haijulikani, pichani kushoto mfanyakazi wa kivuko akiondoa kamba iliyofungiwa kivuko kabla ya watu hawajaisha kuingia na kivuko kimeanza kutoka, nakuwafanya abiria hao kukimbilia kwa kasi huku wengine wakiwa na watoto wadogo.
Kiwango cha Ubebaji wa mizigo ni Cha kutosha kwa kivuko hiki kulingana na idadi ya watu waliopo, hata hivyo kuna vivuko viwili ambavyo hupishana kwa zamu.

ZUNGU ALIVYONASWA KWA RUSHWA DODOMA

Mbunge wa Ilala, Mussa Azn Zungu (kulia) akiwa katika moja ya shughuli za michezo jimboni mwake


WINGU la rushwa limeendelea kutanda katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), na sasa Mbunge wake wa Ilala, Mussa Zungu, anashilikiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), akituhumiwa kutoa rushwa kwa baadhi ya wajumbe wa Jumuiya ya Wazazi.
Zungu ambaye anakuwa mbunge wa pili wa CCM kunaswa na TAKUKURU kwa tuhuma za rushwa, anashikiliwa pamoja na wajumbe wawili wa jumuiya hiyo.

Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge, alikuwa akigombea nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) kupitia Jumuiya ya Wazazi Tanzania Bara na alinaswa juzi sambamba na Dk. Damas Mukasa na Fatuma Kasenga.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Yunis Munisi, alisema Zungu alikamatwa Oktoba 30, mwaka huu, siku moja kabla ya uchaguzi huo.

Akielezea mazingira ya kukamatwa kwao, alisema Zungu alikamatwa akiwa na wapambe wake wanne akitoa rushwa kwa wajumbe ili wampigie kura.

Kuhusu Dk. Mukasa ambaye alikuwa akigombea nafasi ya ujumbe wa Baraza Kuu la Wazazi Taifa na mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM Taifa, Munisi alisema alikamatwa Oktoba 8, mwaka huu, nje ya Ukumbi wa Kilimani mjini hapa kwa kosa la kutoa rushwa kwa wajumbe ili wampigie kura.

Pamoja na hilo, wajumbe wengine wawili nao wanashikiliwa na TAKUKURU kwa kosa la kupokea rushwa kutoka kwa Dk. Mukasa ili wamchague.

Mgombea mwingine aliyekamatwa, Fatuma, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mbeya na Mkutano Mkuu Wazazi Taifa, alikamatwa saa tisa usiku wa kuamkia jana akiwa analipia baadhi ya wajumbe wa mkutano vyakula na vinywaji.

“Inaaminika kwamba huo ulikuwa ni ushawishi ili wajumbe wamchague...alikamatwa katika nyumba ya wageni ya Kitoli iliyopo eneo la Iringa Road mjini Dodoma,” alisema Munisi.

Alisema TAKUKURU imekuwa ikifuatilia taarifa za vitendo vya rushwa tangu kuanza kwa chaguzi za ndani za CCM kuanzia ngazi za chini hadi taifa kwa lengo la kuzuia na kupambana na vitendo hivyo.

Munisi alisema hatua hiyo imefanikiwa kuzuia vitendo vingi ambavyo vilitaka kutendeka baada ya kupata mipango hiyo na kuitibua kabla ya kufanikiwa.

Hata hivyo, alisema changamoto kubwa waliyokumbana nayo ni kitendo cha wajumbe kushirikiana na wagombea na wapambe wao katika vitendo vya rushwa, na hivyo kuwa shida kufanya ushirikiano.

Alisema changamoto nyingine inatokana na wananchi kudai wameona vitendo vya rushwa vikitendeka, lakini hawachukui hatua zozote za kutoa taarifa TAKUKURU.

Kuhusu tuhuma zinazowakabili akina Zungu na wenzake, alisema uchunguzi unaendelea.

Kambi ya Lowassa kidedea
Kambi inayoungwa mkono na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, imezidi kuonesha umwamba wake ndani ya CCM kwa kuibuka kidedea katika uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi uliofanyika jana.

Abdallah Bulembo ndiye ameibuka mshindi wa nafasi ya mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa kura 677 na kuwatimulia vumbi washindani wake, Martha Mlata aliyepata kura 146 na John Barongo aliyeshika nafasi ya mwisho kwa kuambulia kura 43.

Mapema akifungua mkutano huo wa uchaguzi, Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, aliitaka jumuiya hiyo kuchagua viongozi watakaoweza kukiepusha chama na rushwa kwa kipindi chao cha miaka mitano.

“Kiongozi anayehonga ili aweze kupata madaraka huyo si kiongozi na hafahi kuchaguliwa,” alisema Dk. Bilal na kuwataka wagombea wote kuachana na imani ya kutumia fedha kutafuta uongozi.

Aidha, makamu huyo aliwataka wazazi kuwa mstari wa mbele katika kuwalea vijana ili maadili yaliyopotea yarudi kama hapo awali.

Dk. Bilal alisema kuwa wazazi ndio wenye jukumu kubwa la kuwalea vijana na kuwaongoza katika maadili mema, hivyo ni jukumu lao kubwa kuhakikisha vijana wanakuwa na tabia njema.

No comments:

Post a Comment