header

nmb

nmb

Tuesday, December 13, 2011

Sikuiba kura Kabila!!










Rais Joseph Kabila

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila amekanusha vikali madai kwamba alishinda uchaguzi wa nchi hiyo kupitia wizi wa kura.


Waangalizi kutoka wakfu wa Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter walisema matokeo ya uchaguzi huo hayakuwa ya kuaminika, na pia Askofu wa mkuu wa kanisa Katoliki mjini Kinshasa akasema matokeo hayo hayakudhihirisha ukweli halisi.

Bwana Kabila amekanusha madai hayo lakini akakiri kulikuwa na dosari.

Kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi alidai ndiye aliyeshinda.

Watu wasiopungua wanne waliuwawa kwenye maandamano mwishoni mwa wiki ya kupinga matokeo rasmi yaliyompa Rais Kabila ushindi wa 49% dhidi ya 32% aliyopata Bwana Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 78.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Kinshasa, Bwana Kabila mwenye umri wa miaka 40 amepuuzilia mbali madai kwamba matokeo hayo hayakuwa halali.

"Hakuna shaka yoyote, matokeo haya ni halali,'' Bwana Kabila aliambia waandishi.

Alitaja kwamba kura chache alizopata kwenye mikoa ya mashariki mwa nchi hiyo ni dhihirisho kwamba mchakato wa uchaguzi ulikuwa wazi.

Amesema hajashangazwa na hatua ya Bwana Tshisekedi kujitangaza yeye ndiye Rais, lakini akasema ataendelea na kazi yake ya kuiongoza Congo, na kwamba ana imani kuwa uchumi wa nchi hiyo utakuwa kwa kiasi kikubwa katika miaka miwili au mitatu ijayo.

Vyama vya upinzani vimetangaza mipango ya kufanya maandamano baada ya kukataa ushindi wa Bwana Kabila.

Wagombea wengine wanne kwenye uchaguzi huo wamesema lazima urudiwe wakisema kulikuwa na wizi wa kura.
Source:BBC Swahili

No comments:

Post a Comment