header

nmb

nmb

Friday, October 22, 2010

WAHITIMU WA WALSHA YA KIVUKO WAPEWA VYETI!!


Washiriki katika Warsha ya Kivuko (Stepping stone) wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi, Ndg. Modesta Mahiga baada ya kukabidhiwa vyeti vyao.


====== ======= =======

Ilikuwa siku ya furaha na nderemo baada ya vijana kwa wazee wapatao 45 kuhitimu mafunzo ya KIVUKO (STEPPING TONE) ya siku 16 na kukabidhi vyeti vyao. Mgeni rasmi katika mahafadhi hayo alikuwa si mwingine bali kijana machachari, muelimishaji katika masual ya kujitolea katika jamii ndugu Modesta Mahiga , Mkurugenzi wa kampuni ya Proffessional Approach.

Modesta Mahiga, Mgeni rasmi katika mahafadhi haya, pia ni kati ya vijana watatu kutoka Tanzania waliochaguliwa kukutana na Rais Barak Obama wa Marekani alipokutana na vijana kutoka Africa hivi Karibuni. Pia Modesta mwaka huu alipata fursa ya kipekee ya kukutana na wanawake wafanyabiashara, viongozi na waliopata mafanikio makubwa katika Marekani.

Mafunzo haya ya KIVUKO , yalifanyika chini ya uangalizi wa asasi ya Matumaini Group, yalitolewa na Ndugu Onesmo John, muelemishaji, na mwenyekiti wa asasi ya Matumaini Group. Mpango huu wa KIVUKO (STEPPING STONE) umeanzishwa na uko chini ya usimamizi wa DACHEP/PASADA project.

KIVUKO ni mbinu shirikishi jamii inayolenga kuboresha, kukuza, na kuanzishaau kuendeleza mawasiliano na mahusiano, uhamasishaji, uwajibikaji kutoka ngazi ya familia, kaya hadi jamii. Ni mbinu inayosaidia kubaini matatizo, mahitaji na kuyapa kipaumbele, hisia na mitazamo iliyoko katika jamii. Hii ni pamoja na VVU/Ukimwi, Umaskini, kazi gandamizi, unyanyasaji wa kijinsia , matatizo ya kiafya nk, Matatizo ya malezi.

Washiriki walikuwepo wa rika mbali mbali, vijana kwa wazee wakiwemo viongozi kutoka Serikali za mtaa Sinza A , akiwemo Mwenyekiti Ndg. Juma Mgendwa aliyeweza kuhudhuia mafunzo haya ya kivuko kwa siku zote 16. Pia Mama Mtawali, mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi na mjumbe wa serikali za mtaa Sinza A aliweza kushiriki katika mafunzo haya na kukabidhiwa vyeti.

Risala iliyosomwa na mmoja wa wahitimu Ndugu. Zulfa Abdala mbele ya mgeni rasmi, ilikuwa na vipengele mbali mbali kama vile changamoto zilizoko kwenye jamii juu ya VVU/Ukimwi, maneno yenye kushinikiza elimu hiyo iwe endelevu na kunadi kauli yao mbiu, ya KIZAZI KIPYA BILA UKIMWI na huku akiunga mkono kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayosema, Tanzania bila Ukimwi inawezekana.

Akijibu risala hiyo, Mgeni rasmi aliwapongeza vijana kwa kushiriki warsha hiyo na pia kumdhamini na kumchagua na kumpa nafasi ya kuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo. Hii yote inaonyesha wanatambua mchango wake katika jamii.

Alisema elimu hii ya KIVUKO ni muhimu sana na iwe endelevu. Ni elimu ambayo amesema inakuwa vigumu kuipata katika sehemu mbali mbali za mafunzo ya shuleni na katika vyuo.

Pia alisema ushiriki wa viongozi, wakubwa kwa wadogo inaonyesha mshikamano na kuwa elimu hii ya KIVUKO ya suala zima la kupambana na ukimwi ni kwa rika zote. Aliwapongeza viongozi wa serikali za mtaa kwa kuonyesha mfano mzuri kwa kushiriki na vijana wao.

Pia alisema kila binadamu anavipaji visivyopungua 7 hivyo vitumiwe katika kujiondoa katika umaskini na kukabiliana na changamoto mbali mbali zilizoko katika jamii. Pia alijitolea kuja kutoa mafunzo zaidi katika kujitambua na kujua vipaji mbali mbali ambavyo binadamu amezaliwa navyo na jinsi ya kuvitumia katika kujikwamua katika umaskini.

Pia aliipongeza asasi ya Matumaini Group kwa kufanya kazi nzuri ya kuelemisha jamii katika zoezi zima la KIVUKO.Habari picha kwa hisani ya Mtaa kwa Mtaa

No comments:

Post a Comment