header

nmb

nmb

Monday, October 18, 2010

KBC YAIPIGA TAFU NMC!!

Mkurugenzi Mtendaji wa KCB Tanzania Joram Kiarie akimkabidhi Mkuu wa huduma za maabara wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk Emmael Moshi hundi ya milioni 10/- zilizotolewa na benki hiyo leo kama msaada kwa kitengo kinachohudumia wagonjwa hao ili kusaidia uimarishaji wa maabara ya kituo hicho iweze kuhudumia wagonjwa wengi zaidi. Katikati ni Mkuu wa Idara ya Masoko na Mahusiano wa benki hiyo Christina Manyeye.

Mkurugenzi Mtendaji wa KCB Tanzania Joram Kiarie (kulia) akifafanua jambo wakati wa hafla ya kukabidhi msaada wa milioni 10/- kwa kitengo kinachohudumia wagonjwa wenye ‘sickle cell’ cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) leo ili kusaidia uimarishaji wa maabara ya kituo hicho iweze kuhudumia wagonjwa wengi zaidi. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Masoko na Mahusiano wa benki hiyo, Christina Manyeye.


====== ====== ======= =============== ========

KCB yakisaidia kitengo cha ‘sickle cell’ Muhimbili

Na Mwandishi Wetu

BENKI ya KCB Tanzania imetoa jumla ya milioni 10/- kwa kitengo kinachohudumia wagonjwa wenye ‘sickle cell’ cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ili kusaidia uimarishaji wa maabara ya kituo hicho iweze kuhudumia wagonjwa wengi zaidi.

Msaada huo ni wa awamu ya pili ukifuatiwa na wa kwanza wa mwaka 2008 ambapo jumla ya milioni 7.3 zilitolewa lengo likiwa ni kuiwezesha hospitali hiyo kupunguza kiwango cha ugonjwa huo unaoathiri chembe hai za damu.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Mkuu wa Idara ya Masoko na Mahusiano wa KCB Tanzania Christina Manyeye alisema kuwa wameamua kuimarisha maabara hiyo ili angalau kusaidia kupunguza idadi ya vifo kutokana na ugonjwa huo.

“Muhimbili walitufahamisha kuwa ugonjwa huu unatibika ukiwahiwa kwa kutumiwa vifaa maalum. Hili lilitugusa na kuahidi kufanya kazi nao ili kuweza kusaidia maisha ya Watanzania wenzetu kwani bila kusaidia jamii inayotuzunguka uwepo utakuwa na mashaka,” alisema Manyenye.

Kutokana na hilo alisema kama ilivyo kawaida yao kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia wajibu wa kusaidia jamii wataendelea kutoa huduma zinazolenga makundi yote ya watu wakiwemo wafanyabaishara, taasisi za serikali na mashirika mbalimbali, watu binafsi, watoto na wanafunzi.

Kwa upande wake Mkuu wa huduma za maabara wa MNH, Dk Emmael Moshi alisema ugonjwa huo unaoathiri chembe hai za damu kidunia umekuwa ukisababisha vifo vya watu 300,000 kila mwaka kutokana na kukosa matibabu yake.

Akizungumzia takwimu za nchini Dk Moshi alifafanua kuwa kila mwaka watoto 11,000 wamekuwa wakizaliwa na ugonjwa huo wakati asilimia 25 kati yake kama hawakupatiwa matibabu wamekuwa wakipoteza maisha.

“Tanzania ni ya nne kwa kuathiriwa na ugonjwa huo, idadi ya vifo huongezeka kutokana na tatizo la wagonjwa kutofikishwa hospitalini kupatiwa matibabu ya kitaalam kutokana na kupelekwa kwa waganga wa kienyeji kwa kuamini ‘sickle cell’ haitibiki na huisha yenyewe,” alisema.

Ugonjwa huo unaotibika mgonjwa akiwahishwa hospitalini tiba yake ni ufuatiliaji wa kimaabara hivyo kitengo hicho kimewaomba walioathirika nao kufika kwao kupata huduma na kuachana na tabia ya kutumia tiba mbadala.

Mbali ya huduma za kibenki KCB Tanzania imekuwa ikisaidia jamii inayohitaji misaada mbalimbali ili kupunguza umaskini nchini na kwamba misaada hiyo imeelekezwa kwenye sekta za elimu, afya, mazingira na maafa.habari na picha kwa hisani ya blog ya jiachie


No comments:

Post a Comment