BARAZA la Taifa la Usalama Barabarani limeandaa wiki ya Nenda kwa Usalama itakayoanza Agosti 9 hadi 14 mjini Tanga.
Hayo yalisemwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania,Bw. Mohamed Mpinga jana wakati akipokea stika zenye thamani ya sh. mil 50 zilizotolewa na Kampuni ya Zain kushirikiana na Kampuni ya mafuta BP.
Bw. Mpinga alisema wamiliki ambao watashindwa kupeleka magari yao kukaguliwa watachukuliwa hatua na hayataruhusiwa kutembea barabarani mpaka yakaguliwe na kupitishwa kuhakikisha magari yote nchini yanakaguliwa.
"Gari ikikaguliwa na kuonekana nzima mmiliki atapewa hati ya ukaguzi wa gari na stika kuthibitisha gari husika imekaguliwa"alisema Bw. Mpinga.
Alisema magari yatakayokaguliwa na kupitishwa kutembea barabarani yatapewa stika baada ya kulipa sh. 3,000 kwa ajili ya magari madogo ya binafsi na sh. 5,000 kwa magari makubwa ya biashara.
Bw. Mpinga alisema wamiliki wapeleke magari yao kwa hiari katika vituo vya ukaguzi vilivyoandaliwa katika vituo vikuu vya polisi kila mkoa na mkoa wa Dar es Salaam ukaguzi huo utafanyika Polisi usalama barabarani Ilala,Oysterbay na Chang'ombe.
Meneja wa Huduma za Jamii wa Zain, Bi. Tunu Kavishe alisema stika hizo zimetengenezwa kwa ushirikiano na BP ikiwa mchango wa kampuni hizo kuelimisha watanzania kuepuka vifo vinavyotokana na ajali.
Katika hatua nyingine Kamanda Mpinga amesema Mwenyekiti wa Baraza la Usalama barabarani nchini ataendelea kuwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Bw. Abbas Kandoro.
Kamanda Mpinga amesema hayo baada ya wananchi kuhoji sababu za Bw. Kandoro kuendelea kutambuliwa kama Mwenyekiti wa usalama barabarani wakati amehamishwa kuwa mkuu wa mkoa wa Mwanza.
Alisema Bw. Kandoro alipokuwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam aliteuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani,kushika madaraka ya uwenyekiti kwa kipindi cha miaka mitatu inayoishia Oktoba mwaka huu.
"Si lazima Mwenyekiti wa Baraza la Usalama barabarani awe Mkuu wa mkoa ndiyo maana Bw. Kandoro bado ni Mwenyekiti pamoja kuwa amehama" alisema Bw. Mpinga.
Bw. Mpinga aliyerejea juzi kutoka Kondoa mkoani Dodoma kushudia chanzo cha ajali ya lori lililouwa watu 14 katika kijiji cha Mnenia anatarajia kutoa taarifa ya ajali hiyo kesho.
ends...By Peter Mwenda wa Majira
No comments:
Post a Comment