header

nmb

nmb

Thursday, April 1, 2010

MAONYO YA MFUNDAJI BI. SHOSTI .IMELETWA NA MSOMAJI WETU

Madhara ya kuingilia uhuru wa wachumba.

WAPENDWA wasomaji wa safu hii nyeti inayozungumzia mambo mbalimbali yahusiyo jamii, mapenzi na ndoa kwa lengo la kuelimishana.
Leo nipo tena nanyi katika kona hii ili kuendelea kubadilishana utaalam.

Katika mada yetu ya wiki iliyopita nilizungumzia matatizo yanayowakumba vijana wengi wanaotembea na wachumba zao kabla ya ndoa. Nina imani kila mmoja alifurahia mada hiyo. Leo ninawaletea mada nyingine inayozungumzia matatizo yanayotokana na kuingilia uhuru wa wachumba na athari zake.

Nawaletea mada hii kutokana na maswali niliyopata kutoka kwa wasomaji wangu waliotaka kupata ufafanuzi kutoka kwangu. Kama ilivyo ada mimi sina kipingamizi nitawajibu bila wasiwasi.

Kuna wanaodahani kuwa mtu akishakuwa mchumba wake basi ana haki ya kujua siri zake zote au haki ya kuingilia mipango yake.

Maswali niliyoulizwa yatafafnua tatizo hilo, ambapo msomaji wangu mmoja aliuliza kuwa; "Ikiwa hapo mwanzo nilikuwa msichana mtembezi lakini sasa nimeacha, je nikijaliwa kupata mchumba ni vema kumjulisha juu ya hali yangu ili asije akashtuka hapo tutakapokuwa pamoja?"

Jibu: Uchumba ni makubaliano ambayo yanaweza kuvunjika wakati wowote ni vizuri kuchagua kwa makini siri zitakazofaa kumweleza mchumba wako ili hapo baadaye hata kama uchumba wenu utakufa hutakuwa na wasiwasi kwamba siri zako zitatoka nje.
Pengine siri kama hiyo itafaa kuelezana baada ya ndoa ikiwa ni lazima.
Msomaji wangu mwingine aliniuliza swali kuwa; "Mchumba wangu anao marafiki wengine ambao hataki niwajue. Itafaa kweli niendelee kuwa mchumba wake?

Jibu: Ni kwamba ikiwa una hakika kuwa hakupendi na anatarajia kuanza uchumba na marafiki hao ambao hataki uwajue, au ikiwa una hakika kuwa mchumba wako ana tabia mbaya ya kufanya mapenzi na marafiki hao ambao anakuficha, basi yafaa uchumba wenu uvunjike.

Lakini ikiwa uchumba wenu unatambulikana kwa wazazi wenu, hakuna sababu ya kuuvunja . Mnapokubaliana kuwa wachumba sio lazima kila mmoja kuachane na marafiki zake wengine wala sio lazima kila mmoja wenu ajue marafiki wa mwenzake ingawa kufanya hivyo ni jambo linalofaa sana.

Katika uchumba lazima uwe tayari kuthamini uhuru wa mwenzako .
Msomaji wangu mwingine aliuliza swali linalodai kuwa anafanya kazi ofisini. Mchumba wake anataka aache kazi akae nyumbani ambapo ameahidi kumpa fedha mara mbili ya mshahara wake.

Anasema kuwa anampenda kufa na asingependa aone ninaolewa na mtu mwingine, je afanye nini?

Jibu: Ingawa anampenda kufa lakini huna budi kumuuliza au kujiuliza mwenyewe maswali machache. Je ni kwa nini hataki uendelee kufanya kazi?

Je ana mipango ya kukuoa lini? Je uchumba wenu ukivunjika itakuwaje?
Je akifungwa au akiugua au donge analopata likitoweka wewe utakuwa mgeni wa nani?
Je maisha ya kuzurura nyumbani bila kazi ni kitendo cha maendeleo?.

Ni dhahiri kuna kitu mchumba wako anachoogopa ikiwa utazidi kuendelea na kazi yako ofisini. Pengine ana vivu na anahisi huko ofisini una wapenzi wengine.

Pengine ana hofu kuwa utakutana na wengine ambao watakutaka kimapemazi. Kwa vyovyote huyu mchumba hafikirii maslahi yako bali yake mwenyewe.
Ikiwa ameanza kukufuga kwa masharti mapema kiasi hicho,
je mkianza uchumba itakuwaje?
Je akishakuoa unatazamia uhuru wa aina gani. Ushauri wangu ni kuwa huyo mchumba hafai. Achana naye.

Swali lingine linatoka kwa msomaji wangu ambaye anauliza kuwa; "Niko masomoni bado, mchumba wangu ambaye nampenda anataka tuoane mapema. Je niache masomo au nimwache yeye?

Jibu: Kama upo uwezekano wa kuendelea na masomo yako baada ya kuoana hakuna sababu yoyote ya kumwacha .
Vile vile kama unao uhakika kuwa maisha yenu ya ndoa hayatakuwa mazuri ni usikubali kupoteza muda.

Lakini siyo vizuri ukatishe masomo yako kwa kumkimbilia mchumba kabla haujawa na hakika wa maisha yako ya baadaye. Kwa kuwa masomo yana faida kwenu wawili na kwa jamii na nchi nzima, inafaa umtaadhalishe mchumba wako akusubiri umalize masomo.

Ikiwa kweli naye anakupenda bila shaka atakubali. Akikataa na ukaona hana sababu kubwa ya kutaka muoane mapema, basi unaweza kukataa kukatisha masomo yako.

Hapo itakuwa hiari kukuchagua kukusubiri umalize masomo yako au atafute mchumba mwingine. Mara nyingi wachumba wanaotaka kuvunjia wenzao masomo huwa ni wale wenye wasiwasi kwamba huenda wakapigwa teke hapo baadaye.

Kwa maoni zaidi nitwangie kupitia Email gladnessmboma@yahoo.com

No comments:

Post a Comment