header

nmb

nmb

Saturday, April 24, 2010

MAONI YA WADAU WA BLOG YA PR KUHUSU MISHAHARA!!

Mukoba (kushoto)akimwaga maneno kuhusu mgomo.(Picha ya Prona)
KWA miezi kadhaa sasa, kumekuwepo na mjadala mkali nchini unaohusu maandalizi ya mgomo usiokuwa na kikomo kwa wafanyakazi wa nchi nzima, ambao kwa mujibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakzi Nchini (TUCTA), utaanza mapema mwezi ujao.
Kama ilivyotegemewa, taarifa za mgomo huo, ambao wafanyakazi wanataka kuutumia kama silaha yao ya mwisho kudai haki na madai yao ya msingi, zimezua taharuki karibu nchi nzima, kuanzia serikalini mpaka kwa wananchi, maana suala la mgomo wa nchi nzima, tena usiokuwa na kikomo si kitu kidogo ati!
Ndio maana haishangazi kuwa kumekuwepo na vikao kadha wa kadha pamoja na majadiliano ya hapa na pale, vikiwemo pia na vitisho, yote ikiwa ni katika kuhakikisha kuwa mgomo huo usitokee na kusababisha madhara makubwa kwa taifa.
Tukiwa bado katika sintofahamu namna gani serikali inajipanga kutatua matatizo na madai ya wafanyakazi nchini, ghafla serikali imeibuka na waraka unaoagiza sekta binafsi ipandishe mishahara ya wafanyakazi wake kwa asilimia 100.
Pamoja na kuwa zilikuwa habari nzuri kwenye maskio ya watanzania wengi walioko katika sekta binafsi nchini, bado suala hkuwa ilo linaibua masuala na maswali yanayohitaji tafakuri ya kina na kupata majibu.
Kwa mfano kwa nini serikali imeamua kuibuka na suala hili sasa bila ya kuonesha ni kiasi gani waraka wa namna hiyo uliowahi kutolewa miaka michache nyuma ulifanikiwa na waajiri katika sekta ya umma wakauitikia na kuutekeleza kadri ya maelekezo.
Lakini pia kwa muda mrefu sasa, sekta binafsi imekuwa ikilalamikia mazingira magumu ya kuwekeza na kuendesha biashara nchini. Wamekuwa wakitaja maeneo sumbufu kama vile ukosefu wa umeme wa uhakika, miundo mbinu mibovu, rushwa, urasmu serikalini, kodi kubwa, ukwepaji wa kodi, ushindani usio sawa baina ya bidhaa za ndani na za kutoka nje, na mengine mengi.
Masuala hayo yanayolalamikiwa, ambayo hata viongozi wa serikali wamekuwa wakikiri hadharani kuwepo kwake, kwa namna moja ama nyingine yamekuwa kikwazo kwa sekta binafsi kuzalisha kwa tija na hatimaye kumudu kuwalipa wafanyakazi wake vizuri. Maana si jambo linalohitaji utafiti; tija katika uzalishaji ni moja ya sababu za kuwepo kwa viwango vizuri vya mishahara mahali pa kazi.

Hivyo serikali ilipaswa ije na tathmini kuonesha namna gani waraka uliopita ulivyotekelezwa, kwa kiasi gani ulifanikiwa au kukwama, ili kutoka hapo ingeweza kuweka mazingira mazuri ya kuiwezesha sekta binafsi kustawi na hatimaye kumudu nyaraka kama hizo za serikali.

Hilo litawezekana kama serikali itaendesha mambo yake kwa kushirikiana na sekta hiyo (kupitia mpango wa PPP). Vinginevyo tamuko hilo la serikali la wiki iliyopita litachukuliwa kuwa ni mbinu ya kutaka kubadilisha uelekeo wa mjadala, kwamba badala ya kuanza kujadili madai ya TUCTA, wadau wahamishie mawazo yao kwenye mgogoro utakaozuka baada ya sekta binafsi kushindwa kutekeleza agizo hilo la serikali.

Hatuna nia ya kuitetea sekta binafsi, tunasisitiza kuwa wanaowajibu wa kuwalipa vizuri wafanyakazi wao ili nao pia wazalishe kwa bidii kwa ajili ya ustawi wa mtu mmoja mmoja, kampuni, taasisi na hatimaye nchi kwa ujumla, lakini tunachosema ni kuwa serikali ifanye kazi yake ya kuweka mazingira mazuri na pia imalize suala moja baada ya jingine badala ya kutumia ujanja kwa kubadilisha hoja.

No comments:

Post a Comment