header

nmb

nmb

Friday, April 9, 2010



Danguro jingine ambalo Dar Leo imeligundua ni lile lililoko Posta karibu na baa moja maarufu (jina tunalo) ambapo kuna jengo moja ambalo bado ujenzi wake unaendelea na limezungushiwa mabati, hivyo mabinti wanaofanya biashara hiyo ambao wengi wao ni wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu katikati ya jiji wamedai kuwa hulitumia eneo hilo kwa makubaliano na walinzi wa jengo hilo.

Msichana mmoja aliyejitaja kwa jina moja la Faidha mwenye asili ya Kiarabu ambaye ni mwafunzi wa mwaka wa pili katika chuo kimoja hapa jijni (jina tunalo) amesema anafanya kazi hiyo kutokana na kipato kidogo alichonacho wakati matumizi ya chuoni ni makubwa.

Amesema anapopata mteja huenda naye katika jengo hilo na kumpa mlinzi kati ya sh. 500 na sh. 1,000 kisha yeye humalizana na mteja wake.

Pia gazeti hili lilitembelea danguro jingine lililopo Mwananyamala karibu na klabu ya Masai ambako pia kundi la mabinti lilikutwa likiendelea na biashara hiyo kuanzia saa 6 usiku.

Danguro jingine ni lile la Temeke Sokota ambalo wanaotafuta wanawake kwa ajili ya ngono hawahitaji kuumiza vichwa kutokana na kuwapo kwa kundi kubwa la mabinti ambao huvalia mavazi ambayo ni ya aibu kwa jamii.

Dar Leo limegundua kuwa danguro jingine ni lile la makaka poa (bwabwa) lililoko Magomeni. Tofauti na yale mengine, danguro hili linawahusisha wanaume (mashoga).

Madanguro mengine ni lile la Kigamboni lililopewa jina la Uwanja wa Mpira wa huko Italia unaojulikana kama Sanciro ambalo nalo lina mabinti wa aina mbalimbali wenye umri mdogo.

Ingawa wakati wa mchana ni vigumu kugundua kinachoendelea katika danguro hilo, kwa wateja waliolizoea huingia humo mara kwa mara kufanya shughuli zao hizo.

Hata hivyo, kuanzia saa tano usiku wao hubandika bango lao linalosomeka “Karibu Sanciro, Kiingilio 5,000/-”.

Biashara ya hapo ni tofauti na madanguro mengine ambayo msichana hukubaliana na mteja na kisha kwenda kufanya naye ngono na baada ya hapo msichana humlipa msimamizi wa danguro kiasi walichokubaliana.

Katika danguro hilo la Sanciro Kigamboni mteja anapofika huchagua binti anayemtaka na baada ya hapo humlipa msimamizi wao na kisha humchagulia chumba cha kukutana naye.

Msichana aliyejitambulisha kwa jina la Justine lakini akakataa kutaja ubini wake, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari iliyopo Kigamboni (hakuitaja jina kwa kuogopa kufukuzwa), aliliambia gazeti hili kuwa anaifanya kazi hiyo kutokana na maisha ya nyumbani kwao kuwa magumu.

“Marafiki zangu wamekuwa wakinisema shuleni kuwa mimi ni mzuri lakini sina pamba (nguo). Wanasema kama nitapata nguo nzuri nitakuwa mzuri zaidi na wanaume watanipenda zaidi, hivyo kwa kuwa natamani kuolewa ili niondokane na umasikini wa nyumbani na njia nyepesi nikaona ni hiyo kwani napata pesa na raha naipata pia,” alisema Justine.

Hata hivyo, baadhi ya wengine wamesema wanafanya kazi hiyo kwa sababu walipata ujauzito, wakazaa, lakini wakakimbiwa na wanaume waliowapa mamba.

Pia katika danguro hilo kuna baadhi ya mabinti wamedai kuwa wametolewa mikoani kwa kuambiwa wanakuja kufanya kazi za ndani lakini wanapofika mjini wanajikuta wameingizwa katika kazi hiyo.

Danguro lingine liko Buguruni (jina tunalihifadhi) ambalo muda wowote ukitaka huduma utaipata. Katika danguro hilo, siyo mabinti peke yao wanaotoa huduma hiyo, bali hata wanawake ‘ngunguri’ wa mjini.

Nyumba nyingi zenye madanguro huwa ni zile zilizokodishwa kwa ajili ya biashara ya baa, lakini huzikarabati na kuweka vyumba ambako baadhi kuna vyumba viwili kwa ajili ya biashara hiyo kutokana na wateja wengine wanaokunywa pombe na kulewa huhitaji kumaliza shida zao papo hapo.

Nyumba nyingine ni nyumba za makazi ya watu ambazo wamiliki wake huamua kuwapangisha wanawake wengi ambao huduma kama chakula, maji, madawa na vitu vingine vyote vinakuwa juu yake lakini fedha zinatokana na kazi hiyo.

Gazeti hili lilipowasiliana na Kamanda wa polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, kuhusu suala hilo, aliwaomba wananchi waliozungukwa na madanguro hayo watoe taarifa ili wamiliki wake wachukuliwe hatua.

Kamanda Kova alisema ni vigumu kuyasaka madanguro hayo, lakini kwa kushirikiana na wananchi kutakuwa na mafanikio.

By Dar Leo

No comments:

Post a Comment