MOGADISHU,Somalia
VIKOSI vya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) vimerudisha nyuma wanamgambo wa kundi la al-Shabaab kutoka ngome zao kadhaa na kuanzisha vituo vipya 10 mjini Mogadishu.
Msemaji wa AMISOM,Meja Ba-Hoku Barigye alisema juzi kuwa kwa kuanzisha vituo vipya Serikali ya mpito ya nchi hiyo imepata eneo jingine kubwa zaidi.
Mbali na mafanikio hayo,msemaji huyo alithibitisha Uganda kutuma wanajeshi wengine zaidi ya 200 katika mpango huo wa kulinda amani Somalia ikiwa ni baada ya wiki iliyopita vyombo vya habari kumkariri Mkuu wa Jeshi la Ulinzi,Jenerali Aronda Nyakairima akisema kuwa Uganda itapeleka waangalizi wa amani zaidi baada ya kupata msaada wa fedha kutoka kwa Marekani.
“Tutatuma wanajeshi zaidi ya 10,000 lakini itategemea na kama Marekani itatuunga mkono ama la,”alisema.
“Hatutaki kuvuruga bajeti yetu kwa kupeleka wanajeshi wetu na kisha tukaanza kuwalipa mishahara,”alifafanua.
Jeshi hilo la AMISOM ambalo kwa mara ya kwanza kuwasili katika mji huo wa vita wa Mogadishu mwaka 2007 linaundwa na bataliani tano kutoka Uganda na bataliani tatu kutoka Burundi.
Waangalizi hao wa amani ambao wanasaidia kulinda Serikali ya Somalia wengi wao wamewekwa uwanja wa ndege,makazi ya rais na barabara kutoka uwanja wa ndege hadi kwenye makazi ya rais.
Wiki za hivi karibuni wanamgambo hao waliongeza mapambano ili kujaribu kuing'oa madarakani Serikali ya mpito lakini juzi Meja Barigye alisema kuwa kwa sasa wamesonga mbele na kurudisha nyuma wanamgambo hao.(New Vision)
No comments:
Post a Comment