Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Jeshi la Polisi nchini limesema kifo cha askari Polisi WP.7338 PC Suzana kilichotokea katika kituo cha Polisi Tarime tarehe 4/7/2010 kilitokana na tukio la askari huyo kujipiga risasi kifuani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Msemaji Msaidizi wa Jeshi la Polisi Nchini ASP Advera Senso amesema askari huyo WP .7338 PC Suzana siku ya tukio hilo aliingia kazini asubuhi na baadaye kutakiwa kuelekea kwenye lindo kwa muda kuzuia magari yasiingilie msafara wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alikuwa na ziara wilayani Tarime siku hiyo.
Amesema siku hiyo msafara wa rais ulipofika alipokuwa PC Suzana uligawanyika gari la RPC Mara liliacha njia ya msafara na kuingia barabara ya Bomani kwenda ofisi ya DC likifuatiwa na magari mengine matatu likiwemo la Rais.
ASP Senso amefafanua kuwa eneo ulipogawanyikia msafara kuna kilima na kona kali iliyosababisha RPC Mara kupotezana na magari yaliyokuwa mbele yake na hivyo kushindwa uelekeo wa msafara. “Mara baada ya kuona amepotea RPC wa Mara alisimama alipokuwa PC Suzana na kutaka kujua kwa DC ni wapi, akawaonyesha njia ya mkato ambayo haikuwa rasmi iliyopangiwa msafara” amesema.Amefafanua kuwa ilionekana PC Suzana alielewa kuwa RPC Mara alitaka kwenda Ofisi ya DC wakati yeye alitaka kuelewa njia ulipopita msafara.
Baadaye RPC Tarime Rorya alimwagiza mkuu wa kituo Tarime apeleke askari mwingine eneo hilo na PC Suzana arudi kituoni umbari wa takribani mita 100 toka alipokuwa amepangiwa kazi.Amesema PC Suzana alipofika chumba cha mashitaka aliendelea na kazi, baadaye kwa kushirikiana na askari mwenzake PC Dora waliaadaa makabidhiano ya zamu na wakati wakiendelea kuandaa ghafla PC Suzana alichukua silaha moja kati ya mbili zilizokuwa kwenye sanduku na kuingia kwenye ofisi ya mkuu wa kituo na kufunga mlango.
Amefafanua kuwa askari wengine waliokuwa kwenye chumba cha mashtaka walipoona hivyo walikwenda kwenye mlango alipoingilia PC Suzana na kujaribu kuuvunja ndipo akapiga risasi mlangoni na risasi hiyo kutoboa mlango kitendo kilichowafanya kurudi nyuma na baada ya muda walivunja mlango na kumkuta PC Suzana akiwa amejipiga risasi kifuani.
ASP Advera amesema Jeshi la Polisi limechukua hatua za kiutawala na kuboresha mwongozo wa namna ya kusimamia misafara kwenye mikoa ya kipolisi yenye makamanda zaidi ya mmoja chini ya mkuu wa mkoa mmoja, mafunzo kazini na vyuoni kuhusu namna ya kukabilianma na msongo (stress Management). Hata hivyo amebainisha kuwa kifo cha WP Suzana ni suala linalohitaji uamuzi wa kisheria na jalada la tukio hilo limekamilishwa na kupelekwa ofisi ya wakili wa serikali kanda ya Ziwa kwa maamuzi ya kisheria.
No comments:
Post a Comment