header

nmb

nmb

Tuesday, April 6, 2010

WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII ATOA TAMKO KWA WATANZANIA!!

Profesa Mwakyusa akisoma tamko leo asubuhi

TAMKO LA WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII, PROFESA DAVID HOMELI MWAKYUSA ( MB.) KATIKA MKESHA WA MAADHIMISHO YA SIKU YA AFYA DUNIANI, TAREHE 7 APRILI 2010 .

Ndugu wananchi,


Tarehe 7 Aprili kila mwaka ni siku ambayo imeridhiwa na nchi zote wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania ikiwa mojawapo, kuadhimisha Siku ya Afya Duniani. Siku hii huadhimishwa kwa utaratibu uliowekwa na wanachama wa Shirika hilo.

Kila mwaka Shirika la Afya Duniani linatoa kaulimbiu na ujumbe mahususi ambao unalenga kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya suala mojawapo muhimu na lenye manufaa kiafya kwa nchi zote wanachama.

Mwaka huu wa 2010, Siku ya Afya Duniani itaadhimishwa Kitaifa katika jiji la Mbeya, mkoani Mbeya.

Ndugu wananchi,
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani mwaka huu wa 2010 ni, "KASI YA KUKUA KWA MIJI YETU NA CHANGAMOTO ZA KIAFYA KATIKA JAMII".

Kaulimbiu hii imetafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza kuwa ni, "URBANIZATION A CHALLENGE FOR PUBLIC HEALTH".
Kaulimbiu hii inalenga kuhamasisha Jamii kutambua sababu au vishawishi vya watu kuhamia Mijini kutoka vijijini. Sababu na vishawishi hivyo ni vingi. Hapa napenda kutaja baadhi tu ya sababu hizo:-
Kutafuta Ajira kwa lengo la kujikimu kimaisha.



Kutafuta Elimu bora katika Shule za Sekondari, Vyuo na Vyuo Vikuu, ili kuendana na Sayansi na Tekinolojia ya sasa, kwa madhumuni ya kuajiriwa au kujiajiri wenyewe.


Kupata Huduma bora za Jamii k.m. huduma nzuri za Afya, maji na usafiri.


Kutafuta Mazingira mazuri ya kuishi yenye vivutio / vishawishi mbalimbali vya maisha ya kisasa (Modernity). Baadhi ya wahamiaji, huja mjini kwa kushawishiwa na ndugu zao au kwa kuwategemea ndugu zao waishio mijini.


Pia kaulimbiu hii inatukumbusha umuhimu wa kushirikiana na jamii na wadau wote katika kutambua na kukabiliana na changamoto za Kiafya zinazojitokeza kwenye Jamii kwa sababu ya kasi ya kukua kwa miji yetu. Kwa kufanya hivyo tutajijengea uwezo wa kulinda na kutunza Afya ya Jamii endapo changamoto hizo zitajitokeza.


Ndugu wananchi,
Napenda kufafanua kwa kifupi maana ya kukua kwa Miji. Kukua kwa Miji kunahususha ongezeko la idadi ya watu, ongezeko la maeneo ya makazi mijini, kuongezeka kwa mahitaji na huduma za kijamii (k.m. elimu, ajira, afya, maji, usafiri n.k.) kwa watu wanaoishi mijini.


Pia kunakuwa na mzunguko mkubwa wa fedha, shughuli nyingi za kiuchumi, ujenzi wa miudombinu mbalimbali ya maendeleo (k.m. Majengo, barabara, umeme, Viwanja vya Ndege, Viwanja vya michezo, Mahoteli makubwa, Bandari kubwa za kutoa na kuingiza bidhaa mbalimbali, Makampuni makubwa ya Simu n.k.) na haya yote yanayoendana na ukuaji wa sayansi na teknolojia.
Ndugu wananchi,
Tanzania bara kuna jumla ya miji 21. Kati ya hiyo, miji yenye hadhi ya Jiji ni 4 ambayo ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Tanga. Miji yenye hadhi ya Manispaa iko 14 (Arusha, Dodoma, Iringa, Morogoro,


Shinyanga, Bukoba, Songea, Moshi, Musoma, Kigoma, Sumbawanga, Singida, Mtwara na Tabora). Pia kuna mijo mingi midogo.


Kutokana na takwimu za sensa zilizofanyika hapa nchini mwetu, mwaka 1967, 1978, 1988 na 2002, idadi ya vatu, hususan waliokuwa wanaishi mijini imekuwa ikiongezeka kama ifuatavyo:-
MWAKA WA SENSA


ASILIMIA
JUMLA YA IDADI YA WATU
MJINI
VIJIJINI
5.7
94.3

Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2015 (wakati wa tathmini ya Malengo ya Milenio), idadi ya watu watakaokuwa wanaishi mijini itakuwa imeongezeka hadi kufikia watu 13,329,127, sawa na asilimia 28 ya Watanzania wote; na ifikapo mwaka 2025 (wakati wa tathmini ya Dira ya Maendeleo ya Taifa), idadi ya watu watakaokuwa wanaishi mijini itakuwa 19,531,678 sawa na asilimia 31 ya Watanzania wote
Miji yetu inavyokua kwa kasi, husababisha Changamoto za Kiafya, mijini na vijijini katika Jamii yetu kama vile, Mabadiliko ya Tabia Nchi yanayotokana na uharibifu na uchafuzi wa mazingira.


Mabadiliko ya Tabia nchi husababisha Jua na Joto kali, ukame, njaa, Mvua kubwa zinazoambatana na Mafuriko/ Uharibifu wa Miundombinu, kuzuka kwa Magonjwa ya Milipuko n.k. Matukio haya huathiri afya ya jamii kwa kiwango kikubwa.


Hali hii huilazimu Serikali kuhudumia wahanga wa matukio hayo kwa gharama kubwa sana na kudhoofisha juhudi za jamii kujikomboa kiuchumi.


Pia kukua kwa miji kunachangia ongezeko la Magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kama kisukari, magonjwa ya moyo, pumu, magonjwa ya akili, n.k. Maradhi haya hutokana na mienendo ya maisha na tabia za watu waishio mijini kutofanya mazoezi na kula vyakula visivyozingatia lishe bora.


Ndugu wananchi,
Jukumu la kulinda afya ni la kila mtu, familia, kaya na taifa kwa ujumla. Hivyo basi, napenda kuhitimisha tamko langu kwa kutoa rai kwa wananchi wote kujali na kulinda afya zetu:-
kutokana na Changamoto za kiafya katika Jamii zinazosababishwa na kasi ya kukua kwa Miji yetu.


Aidha wadau wote hawana budi kutoa ushirikiano katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za kiafya katika Jamii zinazosababishwa na kasi ya kukua kwa Miji yetu .


Ushirikiano wetu na wadau utatuwezesha kukabiliana na Kasi hii ya kukua kwa Miji yetu na Changamoto za Kiafya katika Jamii ili kuiwezesha jamii kushiriki katika shughuli zao za kiuchumi na maendeleo kwa ujumla.


Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment