WAKULIMA 265 wa Kijiji cha Embukoi Kata ya Siha kati wilayani Siha, Kilimanjaro wamepinga shughuli ya upimaji mashamba yao bila taarifa.
Hatua hiyo imekuja baada ya timu ya wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Siha kufika kijijini humo na kupima maeneo ya mashamba yao yenye ukubwa wa ekari 14,000 kwa ajili ya kugawa kwa watu ambao hadi sasa hawajafahamika.
Timu hiyo iliyohusisha maafisa wa ardhi, uongozi wa wilaya na maafisa kadhaa wa polisi, ilifika kijijini humo Februari mosi, kwa ajili ya upimaji wa mashamba hayo.
Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Embukoi chenye vitongoji vitatu vya Embukoi, Lepolosi na Munge Bw. Lazaro Marko alisema, shughuli hiyo imefanywa bila kutolewa taarifa kwa serikali ya kijiji.
"Sisi wananchi tunapinga zoezi hili la upimaji viwanja kwa sababu tunategemea maeneo haya kwa ajili ya shughuli za kilimo na kufanyia biashara zetu ambazo tunategemea zitatukwamua na hali ngumu aya kimaisha," walisisitiza wakulima hao.
Uongozi wa kijiji uliitisha mkutano maalumu Februari 1na 2 mwaka huu ili kujadili suala hilo ambapo walifikia azimia la kuchukua hatua za kisheria.
Kutokana na hatua hiyo, viongozi hao waliweka pingamizi lililoitaka ofisi ya mkuu wa wilaya kusitisha shughuli ya upimaji wa viwanja hivyo na kutoendelea na shughuli zilizopangwa kufanywa katika maeneo hayo.
Kwa mujibu wa barua ya pingamizi hilo kutoka kwa wakili wao, kampuni ya uwakili ya Shayo, Jonathan & Company, iliyosainiwa na wakili Jonathan Shayo, imetoa muda wa siku 90, kuanzia Februari 8, mwaka huu kusitishwa zoezi hilo.
No comments:
Post a Comment