Bw. Msemakweli akizungumza na mwandishi wa habari wa Gazeti la Majira Bw Kagaruki na Mpigapicha Spear
NENO ufisadi katika elimu linaonekana kuwa msamiati mpya hapa nchini, huku vigogo wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete, wakiwemo mawaziri na manaibu waziri wakitajwa kufanya udanganyifu wa elimu zao.
Tuhuma hizo tangu zianze kutolewa zimevuta hisia za watu wengi huku kukiwa kuna kitabu kilichochapishwa na mwanaharakati Kainerugaba Msemakweli, kikidai kuwa vigogo hao walifanya ufisadi katika elimu zao.
Ingawa baadhi ya anaowatuhumu wamekaa kimya ni wazi kuwa tuhuma hizo zinahitaji majibu. Bw. Msemakweli, anapozungumzia sakata la vigogo wa serikali anaodai walifanya udanganyifu katika elimu waliyopata akidai kuwa huo ni ufisadi wa elimu.
Kwa sasa kijana huyo anaonekana kuanzisha aina mpya ya mapambano dhidi ya wale anaowaita ufisadi wa elimu. Tangu aanzishe mapambano hayo Bw. Msemakweli (33), anaonekana kujipatia umaarufu nchini.
Ujasiri alionao ndiyo umemfanya kufikia hatua ya kuchapisha kitabu chenye picha za mawaziri anaowatuhumu kufanya ufisadi wa elimu. Ujasiri huo unatosha mtu kujiuliza maswali mengi hata kuhoji ni kitu gani anajiamini hadi awasakame viongozi wa serikali iliyopo madarakani.
Ni lazima mtu ajiuliza ni kitu gani kijana huyo anajiamini na kuendelea kushikiria msimamo kuwa mawaziri wa Rais Jakaya Kikwete, wanadanganya kuhusu elimu zao.
Karibu kila Mtanzania anajiuliza kama ana vielelezo vinavyodhibitisha madai yake, ni nani anamfadhili hadi akaweza kuchapisha vitabu na mabango aliyoahidi kuyabandika kwenye barabara kuu za kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam kueleza jinsi vigogo hao walivyofanya ufisadi katika elimu.
Akuzungumza na gazeti hili kwenye mahojiano maalum Bw. Msemakweli anasema kitu cha kwanza kilichomsukuma kuanza kufuatilia shahada na vigogo hao wa serikali ni uzalendo.
"Nilisukumwa na uzalendo ndiyo maana nikafanyakazi hiyo, Tanzania ni mali yetu wote siwezi kukaa kimya wakati watu wanafanya ufisadi katika elimu," anasema.
Anasema utafiti huo wa kubaini udanganyifu wa vigogo hao kuhusu elimu zao ameufanya kwa kipindi kirefu na kujiridhisha kuwa walidanganya.
Anabainisha kuwa yeye na watu aliosaidiana nao walisafiri hadi katika nchi za India na Amerika ili kufuatilia kama kweli vigogo hao walipata elimu katika vyuo wanavyodai kupata elimu zao.
Mbali ya kwenda katika nchi hizo, Bw. Msemakweli anaeleza kuwa walifanya mawasiliano ya kina na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu (UNESCO) ambapo walipatiwa taarifa za kina kuhusu vyuo ambavyo walidai kusoma vigogo hao.
Kwa wale waliodai kusoma vyuo vilivyopo Uingereza, Bw. Msemakweli anaeleza kuwa hawakuwa na sababu ya kwenda nchini humo kwani walikuwa na mawasiliano mazuri.
Anabainisha kuwa kazi ya utafiti wa taaluma za vigogo hao wa serikali aliifanya kwa ushirikiano mkubwa na Taasisi ya Vyuo Vikuu (TCU). " TCU walitupa msaada mkubwa na walitusaidia kuwasiliana na vyuo vilivyopo India na Amerika," anasema.
Akithibitisha jinsi mawasiliano yalivyokuwa mazuri baina yao na TCU, Bw. Msemakweli anaeleza kuwa waliandikia taasisi hiyo barua saba kuomba ufafanuzi wa elimu na vyuo wanavyodai kusoma vigogo hao na kujibiwa kwa barua nane.
Bw. Msemakweli anaeleza kuwa awali walikuwa na orodha ya majina ya vigogo 49 waliotuhumiwa kufanya ufisadi wa elimu,lakini baada ya kufanya utafiti walibaini 19 ndiyo wenye kasoro.
"Baada ya kujiridhisha tukaona kazi ya kwanza iwe ni ya kuwataja hadharani ili kuwatia hasira wakimbilie mahakamani," anasema na kuongeza kuwa katika mkakati wao huo waliamua kutumia mbinu za aina tano.
Anasema mbinu ya kwanza walianza kuitumia Oktoba 10, mwaka jana, ambapo orodha ya vigogo hao ilitangazwa kwenye vyombo vya habari ikielezwa jinsi kuhusu elimu zao.
Anasema alifanya hivyo ili kuwashinikiza wakimbilie mahakamani kumfungulia kesi apate fursa nzuri ya kudhibitishia umma kuhusu jambo hilo.
Anataja mbinu hiyo kuwa ni ya kuchapisha kitabu kinachoeleza kila mmoja kuhusu elimu yake na kuwasilisha vyeti ambavyo anadai ni feki kwenye ofisi za umma.
Anasema tayari vitabu hivyo vinauzwa mitaani kwa bei ya sh. 3,000 akiwa na imani kuwa kabla ya Februali 20, watuhumiwa watakuwa wamechukua hatua ya kumburuta mahakamani.
Anaongeza kuwa ifikapo tarehe hiyo kabla hawajamburuta mahakamani, ataanza kubandika mabango yanayoeleza jinsi suala hilo katika barabara kuu zote zinazoingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Anasema tayari amepata fedha kwa ajili ya kubandika mabango hayo. Alifafanua kuwa tayari mabango hayo yaliyotengenezwa nchini Kenya yamewasili nchini tayari kwa kubandikwa mitaani.
"Mbinu hiyo nayo ikishindikana badala yake wakaendelea kukaa kimya bila kunifikisha mahakamani nitaenda kwenye majimbo yao ya uchaguzi kubandika mabango na kueleza wananchi jinsi viongozi wao hao, walivyo kielimu," alisema Bw. Msemakweli.
"Siwezi kupambana vita hii bila mbinu, vinginevyo watu watasahau," anasema na kuongeza kuwa iwapo vigogo hao watagombea kwenye kura za maoni kupitia CCM kwa ajili ya kuomba ridhaa ya chama kiwaruhusu wagombee ubunge katika basi atapiga hodi kwenye majimbo yao ili kuwaeleza wapiga kura wao kuhusu utata wa elimu yao.
"Nina imani nitawashinda kwani naungwa mkono na nguvu za walalahoi," anafafanua mwanaharakati huyo. Alipoulizwa ni lini ataenda kwenye majimbo yao, Bw. Msemakweli alijibu kuwa ratiba yake itapangwa na kamati yake inayohusika na usalama wake.
Anasema kazi ya kupambana na mafisadi wa elimu inaratibiwa na kamati nne. Anazitaja kuwa ni kamati sheria, uhabarishaji, fedha na ile inayoratibu masuala ya usalama wake.
Kuhusu siasa anasema: "Sina mpango wa kugombea ubunge, nafanya kazi hii kwa kutekeleza wajibu wangu," anasema.
Mbali na kubabiliana na vigogo Bw. Msemakweli anasema kuanzia Machi, mwaka huu watawageukia vigogo wa taasisi 18 za umma ambao walipata nyadhifa zao kwa kutumia vyeti vya uongo na kutoa rushwa.
"Walitoa rushwa wakapata kazi, suala lao nitalipeleka TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), wakishindwa kulifanyia kazi nitatumia mbinu ninazozijua.
Alitoa onyo kwa watu wengine wanaofanya ufisadi katika umri, kwa kudanganya ili wasiweze kustaafu mapema. "Wanafanya ufisadi wa umri ili wasisitaafu mapema, wanawazibia wengine nafasi matokeo yake wanakosa ajira," anasema na kuahidi kushughulikia vigogo hao.
Mwanaharakati huyo alizaliwa Januari 1,1977 Kinondoni Shamba, jijini Dar es Salaam na kupata elimu ya msingi katika shule ya Mwongozo na baadaye masomo ya sekondari Kinondoni Muslim.
Baada ya kuhitimu alichaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha sita katika shule ya Kigoma kabla ya kuhamia Nsumba, mkoani Mwanza. Katika shule hizo anasema alikuwa akiendeleza harakati za kudai haki kama anavyofanya sasa.
Bw. Msemakweli ambaye ni mwanachama wa CHADEMA anasema alianza kuwa na shauku wa kuwa mfuasi wa chama hicho mwaka 1992, baada ya kuhudhuria Mkutano uliohutubiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho, Bw. Edwin Mtei.
Alisema mapambano anayoyaendeleza anatekeleza wajibu wake akiwa mwanachama wa CHADEMA.
ZAIDI SOMA GAZETI LA MAJIRA UPATE UNDANI MWANA HEKAHEKA HUYO
No comments:
Post a Comment